Kweli ndio fimbo ya kukamata

07Dec 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Kweli ndio fimbo ya kukamata

KWELI ni silaha nzuri maishani. Methali hii hutukumbusha umuhimu wa kusema kweli hata kama kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu.

Mechi ya Jumatatu iliyopita kati ya Yanga ambayo sasa yaitwa ‘Timu ya Wananchi,’ na timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) iliniwacha kwenye bumbuazi (mshangao mkubwa unaofanya mtu awe kimya na asijue la kufanya).

Pamoja na bumbuazi hilo, ningali najiuliza kama baadhi ya waamuzi wetu wa mchezo wa kandanda wanaelewa kanuni (sheria ndogo ndogo zilizoundwa kurahisisha utekelezaji wa sheria mama inayosimamia jambo fulani) zote za kuchezesha mchezo huo.

Napata hofu (hisia ya kuogopa) kusema kuwa mechi ile timu zilitoka ‘sare kwa kufungana bao 1-1.’ Binafsi, ingawa ni mwanachama wa Yanga tangu Desemba 2, 1966 kwa kadi namba 447 sikubaliani na sare ile.

Kadi yangu ya nne inayotumika sasa imeandikwa: “Wajibu wa Mwanachama ni kuwa mkweli wakati wote na mwaminifu kwa Klabu.” Natekeleza wajibu wangu ingawa najua kuna watakaonipinga.

Ilisemwa na wahenga kuwa “Kweli ndio fimbo ya kukamata.” Maana yake kweli ni silaha nzuri maishani. Hii ni methali ya kutukumbusha umuhimu wa kuusema ukweli hata kama kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu.

Kadhalika, walisema: “Kweli chungu si uongo mtamu.” Maana yake ni heri kusema ukweli mchungu kuliko uongo mtamu. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuukabili ukweli ijapokuwa una uchungu kuliko kuushabikia uongo.

Kujitapa kuwa Yanga na KMC zilitoka sare kwa kufungana bao 1-1 si kweli bali tunajidanganya mchana kweupe. Kwa mtazamo wangu usio na shaka na ulio sahihi, Yanga ilifungwa 2-1 hivyo washindi ni KMC dhidi ya Yanga.

Najua kuna watakaoguna (kitendo cha kutoa sauti za ndanindani zinazoonesha kutoridhishwa na msimamo wangu), hata kubisha na kuniita ‘msaliti.’ Nimeeleza huko juu kuwa “Kweli chungu si uongo mtamu.”

Waseme watakavyo lakini msimamo wangu ni uleule: Yanga tulifungwa 2-1 na wale vijana wa KMC waliocheza kandanda lililowavutia watazamaji wanaojua kandanda lilivyo.

Kwa wale wanaotazamia ushindi tu hata kama timu haichezi vizuri, nawapa pole. Nawasikitikia kwani watu wa aina hiyo ndiwo waharibifu wa timu kwa kutojua ushindi unavyopatikana. Simo upande wao.

Nilivyo ni kwamba hata timu zangu (Yanga au Taifa Stars) zikishindwa, lakini zilionesha mchezo mzuri, nitazisifu kwani kandanda ni mchezo wa bahati. Timu yaweza kucheza vizuri sana lakini ikapoteza na kuwashangaza wengi.

Bila kuficha wala kumunyamunya (kitendo cha kutikisa midomo kama mtu anayetaka kusema au kucheka), wallahi KMC walicheza mchezo mzuri unaoeleweka kuliko walivyokuwa wachezaji wa Yanga.

Mara nyingi juhudi zao zilizuiwa na walinzi wa Yanga ingawa waliweza kumiliki mpira tangu langoni mwao na kupiga hodi kwenye lango la Yanga, ila bahati haikuwa yao!

Ikumbukwe kuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simba ilicheza vizuri mno dhidi ya Yanga, lakini zilitoka suluhu bila kufungana. Yanga tulishangilia utadhani tulishinda!

Mchezaji aliyeinyima Simba ushindi si mwingine bali ni aliyekuwa mlinda mlango wa Yanga ambaye sasa yupo Simba baada ya kuachwa na Yanga. ‘Kosa’ lake, kama naweza kusema hivyo, ni kipa huyo kudai haki zake yaani bakaa ya fedha za usajili wake Yanga na malimbikizo ya mishahara yake tu basi! Wewe ungekubali?

Turudi nyuma. KMC walionana vizuri kiasi cha wachezaji wao kupiga chenga za maudhi kuanzia mmoja mpaka wanne kuelekea goli la Yanga ila hawakuwa na bahati kama ilivyokuwa msimu uliopita Yanga ilivyoponea chupuchupu kufungwa na Simba mzunguko wa kwanza.

Turudi kwenye mchezo wa Yanga dhidi ya KMC. Katika hekaheka za kutaka kufunga, mchezaji wa KMC aliangushwa eneo la penalti kwenye goli la Yanga, lakini refa hakupuliza filimbi kuashiria penalti kuelekea Yanga!

Tukio lile lilioneshwa na kurudiwa zaidi ya mara tatu na runinga ya Azam iliyorusha mchezo ule mubashara (moja kwa moja) na kuonekana mchezaji wa KMC akichezewa rafu ya wazi kwenye eneo la penalti. Refa ‘akalifumbia macho’ tukio lile!

Vuta hisia kama tukio la kunyimwa penalti wangefanyiwa Yanga pangekuwaje pale uwanjani? Wallahi mwamuzi na washika vibendera wake wangetoka uwanjani kwa ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi.

Mpira uliomfikia mchezaji wa KMC naye kuchezewa vibaya nje ya eneo la penalti ndipo mwamuzi akapuliza filimbi ingawa mpira uliopigwa kuelekea Yanga haukuwa na madhara yoyote kwao.

Kwa kuwa haki ya mtu haipotei, zikiwa zimesalia dakika chache mchezo umalizike, KMC wakapata penalti na kupata bao la kusawazisha kuwa 1-1.

Kama si hivyo KMC ingelala kwa kufungwa bao 1-0. Kama penalti waliyonyimwa ingepigwa, huenda KMC wangetoka uwanjani vifua mbele kwa kuwafunga mabingwa wa kihistoria, Yanga mabao 2-1.

Anayebisha abishe tu lakini ukweli ndio huo. Hata kama kusema ukweli wangu nitanyang’anywa kadi, potelea mbali ninyang’anywe lakini nitabaki kuwa Yanga bila kadi kwani si wote wanaoipenda Yanga wana kadi za uanachama.

Wengi ni mashabiki tu wasiokuwa na kadi zinazothibitisha uanachama wao kwa ‘Timu ya Wananchi.’ Yanga inapoitwa ‘Timu ya Wananchi,’ timu zingine za Tanzania Bara si za wananchi kama ilivyo Yanga?

Kamwe sitokuwa bendera kufuata upepo uendako. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayeyumbayumba kimsimamo au anayefuata mawazo ya watu wengine bila kuwa na msimamo wake mwenyewe.

Habari Kubwa