Waziri atishia kufuta wakala wa mbegu

07Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waziri atishia kufuta wakala wa mbegu

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ametishia kuifuta Bodi ya Wakala wa Mbegu (ASA), endapo itashindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo.

Aidha, ametaka wakala huo kuzalisha mbegu za kilimo zipatazo tani 5,000 katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/20.

Akizungumza jana na watumishi wa taasisi hiyo baada ya kutembelea mkoani Morogoro, alisema pia hatua zitachukuliwa dhidi ya Mtendaji Mkuu wa Wakala.

Amesema pamoja na ASA kuongeza eneo la uzalishaji wa mbegu kutoka hekta 9,890 hadi 10,115.2 bado uzalishaji ni mdogo kwa kuwa inazalisha tani 1,440 pekee huku zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania wanaojihusisha na kilimo wakiwa na uhitaji wa mbegu.

Waziri Hasunga alisema matrekta matatu mapya yaliyonunuliwa na ASA pamoja na zana zake kama vile Boom Spayer, majembe matatu mapya na planter tatu mpya yanapaswa kutumika ipasavyo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora.

"Sisi kama nchi tunahitaji tani 100,086 za mbegu na mpaka sasa hivi uwezo wetu wa kuzalisha ndani na kuagiza nje hauzidi tani 57,000 sasa mahitaji ni makubwa watu wanataka mbegu bora lakini uzalishaji bado upo chini," amesisitiza.

Waziri Hasunga alisema mbegu bora ndio msingi na muhimili wa kilimo hivyo, ili kubadilisha kilimo kutoka kujikimu na kuwa kilimo chenye tija na cha kibiashara ni lazima kuwa na uzalishaji mkubwa wa ndani ya nchi.

Aliongeza kuwa serikali itaiwezesha ASA kuongeza vituo vya usambazaji wa mbegu kutoka vitano ambavyo vinatumika sasa mpaka kuwa vituo 10, ili kuwarahisishia wakulima kupata mbegu katika maeneo yao.

Kadhalika, waziri Hasunga alimtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) kuhakikisha kuwa anatatua changamoto alizozibainisha kwenye taarifa yake ikiwemo ukosefu wa mtaji wa kutosha, kutokuwa na hifadhi ya mbegu ya Taifa, ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji, upungufu wa vitendea kazi na uhaba wa vituo vya kusambaza mbegu.

Changamoto zingine ni upungufu wa magari ya kusambaza mbegu, uchakavu wa mitambo ya kuchakata mbegu, na upungufu na uchakavu wa maghala ya kuhifadhia mbegu.

Habari Kubwa