3TCAA yakiri upungufu marubani wazawa

07Dec 2019
Beatrice Moses
Nipashe
3TCAA yakiri upungufu marubani wazawa

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema nchi inakabiliwa na uhaba wa marubani wazawa na wataalam wa mitambo ya ndege.

Aidha, katika utatuzi endelevu, wameanzisha mashindano ya uandishi wa insha maalum za masuala ya ndege kwa wanafunzi.

Hayo yalibainisha jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Vallery Chamlungu, wakati wa  hafla ya kuwatunza washindi wa insha kuhusu 'Mchango wa Shirika la Ndege la Taifa katika Uchumi wa Nchi'.

Alisema mara kadhaa TCAA inatangaza nafasi za kazi lakini linarudiwa mara nyingi bila kupata wataalam na marubani husika, jambo ambalo linaonyesha kwenye sekta hiyo kuna uhaba wa wanataaluma hao.

Chamlungu alisema shindano hilo la kwanza liliwahusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wenye umri wa miaka kati ya 10 na 13, na kwamba litakuwa endelevu.

"Hii ilitokana na ukweli kuwa, tunatambua umuhimu wa kukuza uelewa wa vijana kuhusu sekta kuanzia ngazi ya chini, ili kuwajengea msingi mzuri kuhusu sekta hii," alisema Chamlungu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kupitia insha hizo, wamebaini kuwa vijana wengi wana ari ya kujifunza kuhusu sekta ya usafiri wa anga na kwamba mamlaka hiyo itaendelea kujenga mazingira ya kuwafikia.

"Tayari kupitia baraza la watumiaji wa huduma za usafiri wa anga, limeanzisha klabu za usafiri wa anga katika sekondari za Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mtwara  na tunaendelea kwenye mikoa mingine," alisema.

Jaji wa shindano hilo, Abubakar Noor, ambaye ni mkufunzi wa mafunzo ya uhandisi wa ndege kutoka Chuo cha Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC), alisema walipokea isha 100 kutoka kwa wananchi katika mikoa mbalimbali nchini.

Alisema pamoja na kupokea insha hizo wakaweka utaratibu wa kupata washindi watano baadha ya mchujo, walitakiwa kuwasilisha maandiko yao katika hafla hiyo, ili kubaini uwezo wa uelewa wao.

Albert Dida aliibuka kuwa mshindi wa kwanza na kuzawadiwa kompyuta mpakato kwa kuwashinda Hazeifa Amirali, Alpha Mbise, Maureen Silayo na Yvonne Lyaruu.  

Hafla hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Dunia (ICAD) ambayo inakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Shirika  la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Habari Kubwa