RAS ahofia wanafunzi kupewa ujauzito kabla ya kuanza shule

07Dec 2019
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
RAS ahofia wanafunzi kupewa ujauzito kabla ya kuanza shule

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, ameingiwa na hofu ya baadhi ya wanafunzi wa kike ambao wamefaulu mkoani hapa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, kushindwa kuripoti shuleni kutokana na kupewa ujauzito.

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kukabiliwa na tatizo kubwa la wanafunzi kupewa ujauzito. Mwaka jana wanafunzi 69 walipewa ujauzito na mwaka huu mpaka sasa taarifa zilizopo ni mimba 120.

Msovela alibainisha hayo jana kwenye kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kuwa kutokana na mkoa kukabiliwa na tatizo hilo, ameingiwa na hofu kuwa huenda baadhi ya wanafunzi  wa kike wasiripoti shuleni kwa sababu hizo.

"Shinyanga ni kati ya mikoa 13 nchini ambayo wanafunzi wake waliofaulu wote wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza. Kama mlivyomsikia jana (juzi) kwenye vyombo vya habari, Waziri (wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani) Jafo akitangaza matokeo hayo, hofu yangu kubwa sijui kama wanafunzi wote wa kike wataripoti shuleni kama hawatakutwa na ujauzito," alisema Msovela.

"Natoa maagizo kwa maofisa elimu ngazi zote, mfuatilie wanafunzi wote waripoti shuleni. Yule ambaye atakutwa amepewa ujauzito kuchueni hatua na kumfuatilia yule ambaye amempatia na kumpeleka kwenye vyombo vya sheria apate kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa watu wengine,"aliongeza.

Akitangaza wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani mkoani hapa. Msovela alisema wanafunzi 23,634, wakiwamo wavulana 11,280 na wasichana 12,354 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Wanafunzi hao ni kati ya 30,393 wakiwamo wavulana 14,322 na wasichana 16,071 waliofanya mitihani hiyo. Waliofeli ni wanafunzi 6,759 ambao niwavulana 3,042 na wasichana 3,717.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba, alisema ili tatizo la mimba za wanafunzi likome mkoani hapa, ni lazima kila mtu atekeleze majukumu yake, wakiwamo walimu wakuu, watendaji wa vijiji, wazazi, polisi, madaktari, mahakimu, kwa kuacha kuharibu ushahidi ili watuhumiwa wafungwe jela.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi, alielezea kusikitishwa na kitendo cha wazazi kuacha kuwapeleka watoto wao wa kike kuishi kwenye shule ambazo zina bweni na kuwapangia mitaani maarufu kama ‘mageto’, hali ambayo alisema imekuwa ikichochea tatizo la mimba za wanafunzi.

Habari Kubwa