Watoto 64 familia duni wafanyawa upasuaji

07Dec 2019
Juster Prudence
Dar es Salaam
Nipashe
Watoto 64 familia duni wafanyawa upasuaji

WATOTO 64 kutoka familia maskini wamefanyiwa upasuaji wa moyo wakati wa kambi maalum ya madaktari 19 kutoka taasisi ya King Salman nchini Saudi Arabia.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi

Upasuaji huo umefanyika kwa ushirikiano na jopo la madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema madaktrai hao waliweka kambi nchini kwa ajili ya kuwezesha upasuaji huo kwa watoto waliokuwa wamelazwa kusubiri matibabu.

Alisema pamoja na watoto hao kufanyiwa upasuaji, bado kuna zaidi ya watoto 500 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji na kwamba unaendelea hadi Desemba 30, mwaka huu kwa watoto 50 kutoka nchini na wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wagonjwa 300,836 wamepata huduma mbalimbali kati yao 1,537 walifanyiwa upasuaji.

Naye Balozi Mdogo wa Saudi Arabia nchini, Abdulaziz Hamad Alasim, alisema nchi hizo zina uhusiano mzuri ambao umesaidia kutoa msaada wa madaktari ili kuwasaidia watanzania wengi kujali hali zao.

"Kama ubalozi tutahamasisha madaktari kutoka nchini Saudi Arabia ili siku nyingine waje wengi zaidi ya waliopo sasa,"alibainisha.

Kwa mujibu wa Balozi huyo, wanatoa misaada kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwamo afya, ujenzi wa vyanzo vya maji na utoaji wa elimu bure kwa wanafunzi wa kitanzania nchini humo.

Aidha, alisema timu ya madaktari wa nchi hiyo walikuwepo nchini walipata ushirikiano mzuri jambo lililowatia nguvu ya kufanya upasuaji kwa watu wengi zaidi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alieleza juu ya mipango yake kwa kushirikiana na taasisi hiyo kupeleka timu ya madaktari kwa ajili ya kuweka kambi mkoani Mwanza kusaidia watanzania wengi wa eneo hilo.

Aidha, aliwataka wazazi, walezi na wadau wa sekta ya afya kujitokeza kuchangia gharama za upasuaji kwa kuwa serikali pekee haiwezi.

Kwa mujibu wa Makonda, gharama za kufanya upasuaji kwa wiki kuwa ni Sh. milioni 465 na kwmaba serikali pekee haiwezi kupata fedha hizo.

Habari Kubwa