Utafiti: Watu wengi wanakula nyama, mboga isiyo salama

07Dec 2019
Juster Prudence
Dar es Salaam
Nipashe
Utafiti: Watu wengi wanakula nyama, mboga isiyo salama

RIPOTI ya walaji wa nyama na mboga nchini imeonyesha kuwa walaji wengi hawana uelewa wa usalama wa nyama, jambo linalowafanya kununua kienyeji bila kujali afya zao.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kulinda Wanyama Duniani iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, watumiaji wa nyama hawajui jinsi gani wanyama wanatakiwa kutunzwa kabla ya kufanywa kitoweo .

Ripoti hiyo ilionyesha asilimia 37.2 ya watumiaji kutoka nchini hawatilii maanani suala la nyama kuchafuliwa na kemikali ambazo zinaweza kuwa hatari kwao.

 Aidha, alisema asilimia 54.37 hawachukulii maanani ustawi wa wanyama  huku asilimia 60.7 na 56.8 wakiwa hawajui kabisa faida za utunzaji au ustawi mzuri wa wanyama katika ukuaji wanyama.

Meneja wa Kampeni ya Utunzaji wa Wanyama Duniani, Dk. Victor Yamo, alisema utafiti uliofanyika ulionyesha kuwa Watanzania wengi wako tayari kulipa zaidi katika ununuzi wa vyakula hivyo ikiwamo nyama kama watahakikishiwa ubora, kama vile kutokuwa na kemikali au viambata vya sumu vya aina yoyote.

Kwa mujibu wa meneja huyo, asilimia 89.9 ya watumiaji hununua nyama na vyakula vinavyotengenezwa kwa nyama katika migahawa na maduka mbalimbali yanayojihusisha na uuzaji wa vyakula nchini.

Pia alisema tathmini hiyo inaonesha kuwa asilimia 38.2 ya watumiaji hao wangeweza kununua zaidi kama kungekuwa na mazingira mazuri ya utengenezaji wa vyakula hivyo.

Dk. Yamo alisema ipo haja ya kutoa elimu kwa watumiaji wote pamoja na wauzaji wa vyakula juu ya ubora wa nyama tutakayopata kama tutazingatia ustawi wa wanyama hao ikiwa ni pamoja na mazingira wanayotegemea kwa ajili ya ukuaji.

 Alibainisha kuwa elimu pekee haitatosha kubadili taswira hiyo kama hakutakuwa na sheria maalum zinazolinda ustawi wa wanyama na usalama wa vyakula.

Mtaalamu huyo alifafanua kuwa lengo la kampeni hiyo siyo tu kuwalinda watumiaji bali kuhakikisha Tanzania inafikia viwango vya kimataifa katika ubora wa vyakula.

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa asilimia 53.3 ya Watanzania wanatumia dawa za kuua wadudu katika mashamba yao ili kupunguza upatikanaji mbovu wa mazao huku asilimia 79.4 ya watumiaji wakiwa na imani ya kwamba dawa za kuua wadudu kwenye mazao huchangia kuongeza kemikali katika mazao.

Aidha, alisema asilimia 87.8 ya watumiaji wakielezea kuona madhara yanayosababishwa na ustawi mbaya wa wanyama ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa nyama isiyo na ubora huku asilimia 61.8 ya watumiaji wamesema wako tayari kuongeza malipo kwa ajili ya nyama itakayotengenezwa kwa viwango.

Habari Kubwa