JPM akerwa mvutano upanuzi wa hospitali

07Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM akerwa mvutano upanuzi wa hospitali

RAIS John Magufuli ameonyesha kukerwa na mvutano wa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita ambao wametumia muda mwingi kubishana kuhusu upanuzi wa majengo ya hospitali ya Chato licha ya Sh. Bilioni moja kutolewa.

Kutokana na mvutano huo, ameagiza upanuzi wa hospitali hiyo ufanyike mara moja kwa kuwa fedha zipo.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana baada ya kutembelea hospitalini hapo na kuwapa pole wagonjwa akiwamo Mzee Zephania Kanoge ambaye ndiye aliyemhamasisha kuingia katika siasa mwaka 1995.

 “Serikali haiwezi kuvumilia kuona watu wakipata shida kwa uzembe wa viongozi wachache wa walmashauri. Viongozi wa halmashauri hii hakikisheni mnaanza mara moja upanuzi wa majengo haya kwa kuwa serikali imeshatoa fedha za ujenzi tangu mwezi Julai mwaka huu,” alisema kupitia taarifa iliyotolewa na Ikulu.

Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke, kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unafanyika na kwa gharama zinazostahili.

Pia amemtaka Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Ligobeth Kalisa, kuhakikisha mashine ya X-Ray inafanya kazi muda wote na wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati.

“Si sawa kwa Hospitali ya Wilaya kukosa huduma za X- Ray eti kwa sababu hakuna mikanda ya kupigia picha,” alisema.

Kuhusu historia ya mzee Kanoge, taarifa hiyo ya Ikulu ilisema yeye na mwenzake Constantine Misungwi (sasa marehemu), walimfuata Rais Magufuli mara mbili jijini Mwanza alikokuwa akifanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza wakimtaka agombee ubunge.

“Licha ya kukataa, wazee hao waling’anga’ania hadi alipokubali na wakabeba jukumu la kumfanyia kampeni kwa kutumia pikipiki hadi aliposhinda uchaguzi,” ilisema taarifa hiyo.

Baada ya kumjulia hali, Rais Magufuli alimshukuru mzee hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maisha yake ya siasa na amemuombea apone haraka ili aweze kurejea nyumbani na kuungana na familia yake.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli aliwaona wagonjwa wengine pamoja na wanawake na watoto waliofika kupata chanjo na kuwahakikishia kuwa serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za afya.

Habari Kubwa