JPM: Mafisadi bado wapo, tutawakamata

09Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
JPM: Mafisadi bado wapo, tutawakamata

RAIS John Magufuli amesema mafisadi katika serikali ya awamu ya tano bado wapo, na kwamba ataendelea kuwashughulikia mpaka watapike fedha zote.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, jijini Mwanza, katika hafla ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa meli mpya ya kisasa, chelezo na ukarabati wa meli ya Mv Victoria na Mv Butiama.

Alisema miradi hiyo ilicheleweshwa kwa kipindi kirefu kutokana na fedha kutafunwa na mafisadi.

"Ni lazima tuzungumze ukweli, kwamba ni lazima tufanye mabadiliko ya kweli kusaidia nchi yetu, kwa nini tuweze sasa na kwa nini ishindikane miaka yote hiyo?" Alihoji Rais Magufuli.

Akizungumzia ujenzi wa meli mpya, Rais Magufuli alisema zaidi ya miaka 20 baada ya kuzama kwa meli ya Mv Bukoba ilitakiwa kujengwa meli nyingine, lakini jambo hilo halikufanyika.

"Kama mnavyofahamu baada ya kuzama kwa Mv Bukoba kumekuwa na tatizo kubwa la usafiri kwa wanaozunguka Ziwa Victoria, nilipokuja katika kipindi cha uchaguzi mwaka 2015 niliahidi kununua meli na sikujua pesa nitatoa wapi."

"Niliwaza kwamba kama wengine wote waliopita hawakununua, mimi nitawezaje, lakini kumbe inawezekana, pesa zipo nyingi ila zinachezewa na mafisadi ambao hata sasa wapo, hawajaisha."

"Hivi sasa tunafanya mpango wa kujenga pia standard gauge (reli ya kisasa) kutoka Mwanza hadi Isaka, sasa msiniulize pesa nitatoa wapi, nitaendelea kubanana na mafisadi mpaka watapike zote."

Katika ujenzi wa meli hiyo na ukarabati wa Mv Victoria na Mv Butiama, Rais Magufuli alisema miradi hiyo kwa ujumla wake itagharimu Sh. bilioni 153 ambazo ni fedha za ndani. 

Alizitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa miradi hiyo, kuhakikisha kwamba inazalisha faida. 

Alisema katika kipindi cha uongozi wake hataki kusikia chombo chochote kinachojiendesha kwa hasara.

"Kwenye serikali yangu kitu kinachoitwa hasara ameshakufa zamani, kwangu mimi anayeishi ni faida tu, kwa hiyo nataka mhakikishe miradi hii yote inazalisha," alisema Rais Magufuli.

Pia aliagiza miradi hiyo kukamilika kwa wakati ili kusaidia kutatua tatizo la usafiri katika Ziwa Victoria.

"Nimeambiwa ukarabati wa chelezo umekamilika kwa asilimia 68, Mv Victoria asilimia 65 na Mv Butiama asilimia 60, hii inanipa uhakika kwamba miradi hii itakamilika kwa wakati uliopangwa na ikiwezekana hata kabla ya wakati ili kutatua tatizo la usafiri katika ziwa hili la Victoria," alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia kuanza kwa safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Moshi mkoani Kilimanjaro, Rais Magufuli alisema ni jambo la kushangaza huduma hizo kisimama kwa kipindi kirefu.

"Na hii lazima tuzungumze ukweli, miaka 26 yote huduma za treni katika mkoa huo zilikuwa zimesimama. Siyo kwamba hakukuwa na pesa, isipokuwa hatukujipanga, hatukuona priority (kipaumbele) kwa pesa tunazokusanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, huo ndio ukweli."

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi, alisema meli mpya itakuwa na madaraja matatu na kwamba ya kwanza itakuwa inabeba abiria 50, la pili abiria 316 na la tatu abiria 834.

Hamissi alisema itakuwa inafanya safari zake Mwanza, Bukoba, Musoma na nchi jirani za Kenya  na Uganda.

Hamissi alisema, makandarasi wanaotekeleza  miradi hii kwa upande wa ujenzi wa meli mpya ni  Gas Entec akishirikiana na KANG NAM zote kutoka Korea ya Kusini  pamoja na SUMA JKT ya Tanzania, ujenzi wa chelezo mkandarasi ni Stx Engine anashirikiana na SAE KYUNG zote za Korea Kusini, huku mkandarasi wa ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama ni KTMI nayo kutoka Korea ya Kusini. 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwaagiza makandarasi wanaosimamia miradi hiyo kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa ubora na ikiwezekana waikamilishe miradi hiyo kabla ya wakati.

"Wana-Mwanza jipangeni vizuri katika kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na serikali inawanufaisha, huku viongozi wote wa mikoa ikiwamo Mwanza kuhakikisha mnawahamasisha wananchi katika suala hilo," alisema.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Elizabeth Faustine na Neema Emmanuel, MWANZA

Habari Kubwa