Faini 300,000/- wasiopeleka shule waliochaguliwa kidato cha kwanza

09Dec 2019
Gurian Adolf
Katavi
Nipashe
Faini 300,000/- wasiopeleka shule waliochaguliwa kidato cha kwanza

SERIKALI mkoani Katavi imeagiza kukamatwa na kisha kutozwa faini ya Sh. 300,000 au kwenda jela miezi miwili wazazi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza Januari 2020 na kushindwa kuwapeleka shule.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera, wakati akizungumza katika kikao cha bodi ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwakani baada ya kuhitimu na kufaulu mitihani yao.

 Aliagiza kuwa wanafunzi wote waliopangiwa  kujiunga kidato cha kwanza ambao watashindwa kwenda shule wazazi wa watoto hao ni lazima wakamatwe na watozwe faini ya Sh. 300,000 au kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi miwili.

Alisema mkoa huo utaanzisha mahakama zinazotembea kwa ajili ya kuwahukumu wazazi wa watoto ambao watakuwa wameshindwa kuripoti shule na watahukumiwa huko huko waliko.

Aliagiza pia hataki kusikia katika mkoa huo kuna mwanafunzi  anasoma akiwa amekaa chini  kwani watakuwa hawamtendai haki Rais John Magufuli  aliyeanzisha utaratibu wa elimu bila malipo.

Aliwataka wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kushirikiana na serikali za vijiji zenye hifadhi za misitu pamoja na wakala wa misitu TFS ili watoe kibali cha kuvuna mbao kwa ajili ya kutengeneza madawati  kwenye shule ambazo zitakuwa na upungufu wa madawati.

 Aliwaonya baadhi ya wazazi ambao wamekuwa na tabia ya kutaka watoto wao kwenda shule ili waolewe waache tabia hiyo mara moja kwani watakaobainika kufanya hivyo yeye kama mkuu wa mkoa atawachukulia hatua kali za kisheria.

Homera alisema   wanafunzi wote waliomaliza darasa la saba na kufaulu watakwenda sekondari, na wale wasiofaulu  watapangiwa kujiunga na vyuo vya ufundi hivyo hakuna mtoto atakaye kuwa akizurura ovyo mitaani.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi,  Abdalla Malela,  alisema mkoa huo unatarajia kukamilisha ujenzi wa shule saba za sekondari za kata ifikapo Januari 15  kitendo kitakachosaidia wanafunzi kuepukana na tatizo la kusoma katika shule zilizo mbali na makwao.

Alizitaja shule hizo za kata kuwa ni  Sekondari ya Kasekese, Kakoso, Kakese, Itenka, Ugala, Senkwa na Ilunde.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa  Katavi, Newaho Mkisi,  alisema jumla ya wanafunzi 8,510 wamechaguliwa kujiunga  na shule za sekondari za kutwa wasichana wakiwa 4,281 na wavulana 4,229 na waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni 31, wavulana 22 na wasichana tisa na wafunzi wanane wamechaguliwa kujiunga na shule zenye mahitaji maalum.

 Alisema ufaulu wa wanafunzi kwa mkoa huo umeongezeka kwa asilimia  7.07 na kuufanya mkoa huo kupanda katika ufaulu wa kitaifa kutoka nafasi ya tisa ya mwaka jana hadi kuwa katika nafasi ya tano kitaifa mwaka huu.

Diwani wa Makanyagio, Haidari Sumry alisema idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na shule za bweni kutoka katika mkoa huo ni chache, hivyo mkoa ungeangalia namna ya kuanzisha shule moja ya sekondari ya kutwa ambayo itakuwa ikiwachukua wanafunzi wenye ufaulu wa juu.

Habari Kubwa