Mchawi ni mlezi

10Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Mchawi ni mlezi
  • Ni madereva wa boda, daladala, makonda wageuka walinzi, watetea mabinti mitaani

KWA muda mrefu lawama za kuwarubuni mabinti kuanzia watumishi wa ndani, wanafunzi na wasichana kwa ujumla zimekuwa zikielekezwa kwa madereva na makondakta.

Madereva wa bodaboda na daladala, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kupiga vita rushwa ya ngono.

Wanaolaumiwa ni madereva na makondakta wa daladala mijini na vijijini,  mabasi ya abiria mikoani  tuhuma nyingi zaidi zinaelekezwa kwa  bodaboda.

Hawa ndiyo ambao kutokana na kuwa na usafiri wakati wote, fedha za papo na kujiona kuwa wana umuhimu wa kipekee katika jamii kutokana na huduma wanazozitoa, wamekuwa chanzo cha kuwalaghai wasichana na kuwatumia kingono hata kuwapa mimba.

Lakini kama wahenga walivyosema "mchawi mpe mwanao amlee", wakimaanisha kuwa kufanya hivyo kutasababisha mchawi aogope kumdhuru mtoto huyo.Ataogopa kumloga kwa sababu ya kuhofia kwamba atajulikana kuwa  yeye ndiye aliyehusika katika tukio hilo, hivyo akikabidhiwa, atahakikisha mtoto anakuwa salama na kulindwa muda wote.

Msemo huo unaweza kulinganishwa na kile sasa kinachofanywa na baadhi ya madereva wa bodaboda na daladala, ambao wamekuwa wakituhumiwa kuwarubuni wanafunzi kwa lefti zinazolenga kufanya nao ngono ambazo huishia kuwapa ujauzito, ndoa za utotoni na  maradhi , yote hayo yakikatisha ndoto za wasichana kusoma na kuhitimu kitaalamu.

Jijini Dar es Salaam, madereva takribani  800 wakiwamo pia makondakta wa daladala wamegeuka kuwa walezi na wanaotekeleza jukumu la kuwaelimisha na kuwalinda mabinti hasa wanafunzi dhidi ya uharibifu wowote unaotokana na ngono.

Wanawahamasisha, madereva wenzao na jamii kwa ujumla ili kuwalinda na kuepuka kuwarubuni wanafunzi na kufanya nao mapenzi.

Kazi hiyo wanaifanya chini ya taasisi ya kijamii ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (Wajiki) ya jijini  ambayo imejikita kwenye wilaya za Kinondoni na Temeke.

JUKUMU JIPYA

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Janeth Mawinza, aliyewaibua madereva hao, anasema, kabla kuwapa majukumu, alianzia kwa kuunda klabu za wanafunzi wa kike kwenye baadhi ya shule za msingi wilayani Kinondoni.

"Lengo lilikuwa ni kutaka kujua matatizo yanayowakabili wanafunzi wa kike kuanzia nyumbani, mitaani na hata shuleni, ndipo wengi wao wakaeleza  kuombwa rushwa ya ngono madereva wa bodaboda na daladala," anasema.

Anasema, klabu hizo zilianza mwaka 2015, na alipobaini hilo, yeye na timu yake waliandaa utaratibu wa kutembelea vijiwe mbalimbali vya madereva wa bodaboda na daladala ili kuwaelimisha.

"Elimu yetu ilikuwa ni kuhusu madhara ya rushwa ya ngono ambayo mwisho wake inaweza kuwa ni mauti kwa mwanafunzi au hata kwa dereva mwenyewe, hivyo tukawaomba waache tabia hiyo," anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, baadhi ya madereva waliipokea elimu hiyo na kuanzia kuwa mabalozi wa wenzao na kuanza rasmi kazi ya kuelimisha wenzao mwaka 2018 chini ya Wajiki.

"Hadi sasa wapo zaidi ya 800 wakifanya kazi kwenye Kata ya Makumbusho, wilayani Kinondoni na Mbagala Wilaya ya Temeke na tunatarajia kuingia Wilaya ya Ilala, Machi mwa kesho," anasema.

Anasema, madereva hao wameunda kamati zao za ulinzi ambazo huwa kwenye vituo vya mabasi, wakiwaona wanafunzi wanazagaazagaa wanawafuata na kuwauliza ili kujua matatizo yao.

Mawinza anasema, iwapo mwanafunzi atakuwa ana tatizo la nauli au anazuiliwa kupanda gari, wanamsaidia ili awahi nyumbani, na kama hana sababu za msingi, wanamkamata na kumpeleka kituo cha polisi.

"Yaani kinachofanyika ni sawa na usemi wa "mchawi mpe mwanao amlee", kwani wale ambao wamekuwa wakilalamikiwa kuwarubuni wanafunzi, ndiyo wanafanya jukumu la kuwalea, na wamesaidia sana, " anasema.

Anasema, wiki iliyopita kulikuwa na mwendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo madereva hao ili kuwa mabalozi katika kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, ambazo zinamalizika wiki hii, ili wafanye kazi hiyo kwa ufanisi.

KUJITAMBUA

Mkurugenzi Mawinza anasema, taasisi yake imechukua hatua hizo, ili kuhakikisha pande hizo mbili zinajitambua na kuvunja ukimya na kuwafanya wanaomba rushwa ya ngono waache, na waombwaji nao wabadilike na kutoa taarifa.

"Ikumbukwe kuwa rushwa ya ngono ina madhara mengi kwa wanafunzi ikiwamo udhalilishaji utu wa mtu na pia inauma na kuondoa nguvukazi ya taifa ambayo ni vijana, kwa kuambukizwa magonjwa ukiwamo Ukimwi," anasema.

Anasema, rushwa na ngono hasa kwa mabinti ni hatari kwa kuwa wengine hujikuta wakipata mimba zisizotarajiwa na hivyo kupata madhara makubwa wakati wa kujifungua kwa kuwa viungo bado havijakomaa.

"Wanaopata mimba za utotoni pia huathirika kisaikolojia, hivyo ni muhimu kuwalinda, ndiyo taasisi yetu inashirikiana na madereva hawa, ambao kwa muda mrefu wanalalamikiwa kuwarubuni wanafunzi," anasema.

Anasema, Sera ya Elimu Bure inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo imetoa fursa kwa watoto wengi wa kike kuandikishwa shuleni, ni muhimu jamii kusaidia kuitekeleza kwa kumlinda mtoto wa kike.

"Umbali mrefu na tatizo la usafiri kwa wanafunzi ni mojawapo ya sababu zinazochangia kuendeleza ukatili wa kingono kwa watoto wa kike wakiwamo wanafunzi, hivyo ni muhimu kuwa na mbinu za kusaidia," anasema.

KWA MADEREVA

Dereva wa bodaboda ambaye pia ni mjumbe kutoka Wajiki, Khalfan Chusi, anasema baada ya kupata elimu, sasa wanaisambaza kwa madereva wenzao ili kuhakikisha wanafunzi wa kike hawarubuniwi.

Ukweli ni kwamba mchezo wa baadhi ya madereva kuwarubuni wanafunzi na kuwageuza kuwa wapenzi wao kwa sababu ya lifti ulikuwepo sana, lakini ninaamini unaanza kupungua," anasema Chusi.

Chusi anasema, hiyo inatokana na wao ambao wako chini ya Wajiki kwenda kwenye vijiwe na mitaani kutoa elimu ya kumnusuru mtoto wa kike dhidi ya rushwa ya ngono.

"Lakini pia broo nikwambie, wapo baadhi ya watoto wa kike wameshindikana kwao, hao wanaweza kukuambia macho makavu kuwa uwape lifti halafu mtamalizana, sasa ukiwa mwepesi utakubali," anasema.

Naye dereva wa daladala inayofanya ruti zake kati ya Mbagala na Kawe, Albert Shoo anasema, wanawake na wanafunzi ni waathirika wakubwa wa rushwa ya ngono, kutokana na shida ya usafiri jijini Dar es Salaam.

"Unaweza kuwakuta bado wanasota kituoni unampakia mmoja, hawezi kukataa, unamsomesha unaenda kufanya naye mapenzi kirahisi, lakini biashara hiyo haifai kufanywa na watu wanaojitambua," anasema Shoo.

Kwa upande wa Salum Hamza ambaye pia ni dereva wa daladala inayofanya ruti zake kati ya Makumbusho na Bunju, anasema mwanafunzi anapofika shuleni kwa wakati na kusoma kwa wakati ni jambo la msingi.

"Sisi hapa Makumbusho tumejiwekea utaratibu kwamba ni lazima kila daladala ichukue wanafunzi wanne, hatutaki wanyanyasike na wanaoshangaa vituoni bila sababu tunawakamata," anasema Hamza.

Anafafanua kuwa wakiwapo wanafunzi wa aina hiyo, huwafikisha kwenye ofisi za serikali za mitaa au polisi, lengo kuu likiwa ni kusaidia kuwaepusha na mambo ya rushwa ya ngono na hata vitendo vya ulawiti.

"Elimu hii ya Wajiki tuliopata imetusaidia sana, mimi hapa nilipo hata nikienda Tandika au kwingine nikakuta mwanafunzi wa kike ananyanyaswa na kondakta ama dereva, ni lazima niingilie kati kumsaidia," anasema.

Habari Kubwa