Utolewe ufafanuzi zaidi kuhusu mahakama Afrika

10Dec 2019
Anil Kija
Nipashe
Utolewe ufafanuzi zaidi kuhusu mahakama Afrika

WASEMAJI wa masuala ya sheria na katiba  nchini wamekuwa na kazi ya ziada hivi karibuni ya kutofautisha kati ya serikali na wasimamizi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Wananchi.

Majaji wa Mahakama ya Afrika wakiwa kwenye makao makuu ya taasisi hiyo yaliyoko Arusha. PICHA: MTANDAO

Suala ni licha ya kuwa mahakama hiyo iliundwa na maskani yake yakawa Arusha mapema miaka ya 1980, zipo tofauti kati ya mpangilio wake na utendaji wake.

 Mara nyingine utendaji hufuata mawimbi ya kiitikadi yanayovuma wakati huo  na siyo mpangilio halisi wa kuundwa kwake karibu miaka 40 iliyopita.

Ndicho anachojaribu kueleza Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro, kupitia vyombo vya habari, wakati suala hilo linavuma safari hii.

Anasema kanuni ya msingi ya mahakama hiyo ni kufuata mlolongo wa kisheria katika nchi halafu ikiwa imeukamilisha na kuna malalamiko au rufani inatakiwa, ndipo mhitaji anaweza kufungua shauri katika mahakama hiyo.

 Kinachotokea ni kuwa wahusika wanaotaka kupeleka kesi  mahakamani dhidi ya serikali wanaeleza kutokuwa na imani na sheria au hata mahakama za nchi na kwa maana hiyo mahakama hiyo ya kimataifa inakuwa kimbilio halisi.

Anayejua diplomasia inavyoendeshwa anaelewa kuwa Mataifa ya  Umoja wa Afrika (AU) hazingeweza kuunda mahakama mbadala wa mfumo wa mahakama wa nchi zao ila kuweka chombo kingine ambacho kinaendana kwa kiasi kikubwa na mifumo yao.

Kwa vile Mahakama ya Afrika ina kitu kama nafasi ya uhakiki na mapitio ya kile kinachofanywa na mahakama za wanachama wa AU tofauti katika mausala yanayaogusa haki za binadamu, ni lazima kuwe na misingi au angalau marejeo ya pamoja ya kiitikadi.

 Wakipishana sana inakuwa vigumu kuendesha mazungumzo, ndiyo hapo nchi inaamua kujitoa katika utaratibu huo kwa muda, hadi tofauti hizo zitakapoangaliwa upya.

Wanachosema wanaohoji katika mazungumzo na Dk, Ndumbaro ni kuwa kesi nyingi zimekuwa zikipelekwa katika mahakama hiyo moja kwa moja na kupokelewa, hali ambayo inaashiria mojawapo kati ya masuala au vipengele vya aina mbili katika uendeshaji wake.

Kipengele kimoja cha kufikisha kesi kwenye Mahakama ya Afrika bila kupitia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kinaweza kuwa ni kupewa uwezo msajili wa kesi au Msajili wa Mahakama kuwa na uwezo wa kuamua kupokea kesi au kuikataa.

 Ina maana kuwa halazimiki kuhitaji mrejesho wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani kwanza.

Hatua nyingine ya kuanzia ni lazima iendana na ile ya kwanza pale mlalamikaji anapokubaliwa na mahakama  kuwa sheria za nchi husika, kwa ujumla wake au katika kipengele maalum kinachogusa haki za binadamu, ni kinyume dhana au itikadi ya kuundwa kwa Mahakama ya Afrika.

 Ina maana shauri likipelekwa huko ni sawa na bure kwani halitasikilizwa kwa kanuni zinazotambuliwa na mahakama hiio. Siyo za nchi tena.

Unaweza kujiuliza ni vipengele gani vilikuwepo wakati Mahakama ya Afrika inaanzishwa, na kukubaliwa (akiwa mwenyeji) na Waziri wa Sheria na Katiba wakati huo, Joseph Warioba, na miaka kadhaa baadaye akiwa amemaliza kipindi chake cha uwaziri mkuu akawa jaji katika mahakama hiyo. Sasa ni kwa msingi wa sheria zipi Jaji Warioba alikuwa mwenyeji katika uanzilishi wa mahakama hiyo na baadaye kuwa jaji, halafu mmoja wa warithi wake baadaye anaona hana njia ila kulishauri Baraza la Mawaziri kuwa Tanzania ijitoe kwa muda hadi mfumo wa kisheria umewekwa sawa?

 Jibu rahisi ni kuwa yako mabadiliko, ya mwelekeo wake kiitikadi. Kuwekwa kipengele cha kumaliza mfumo wa kisheria au mahakama ndani ya nchi kabla ya kuhitaji msaada katika mahakama ya kimataifa ni jambo la kawaida, lakini mahakama hizo kwa kawaida pia zinakuwa na uhuru wa kukubali kesi bila mrejesho unaokubalika kutoka mahakama za nchi husika.

Kutaka mrejesho ni kama kuomba kibali kuwa shauri hilo lipokelewe, wakati kila mahakama au jopo la kisheria huwa na mifumo ya kisheria ya kukubali au kukataa shauri kutoka popote.

 Ina maana kuwa nchi inaweza kutia saini ‘protokali’ ya kuundwa kwa mahakama kama hiyo (ya kimataifa) na huku ina mashaka na vipengele kadhaa. Endapo haitatokea mikwaruzano dhahiri, nchi hiyo inaendelea na uanachama ikijua mahakama hiyo iko huru na endapo itafikia mahali kutokuelewana kunaongezeka, inaweza kuondoa saini yake kwa muda kwa tafakuri zaidi.

Katika lugha ya kisheria na kidiplomasia, nchi inapoitaka mahakama ya kimataifa ijitafakari kuhusu jinsi inavyofanya kazi, inachosema ni kuwa yenyewe imejitafakari imeona kuwa kuna tofauti za kina kati ya matazamio yake na utendaji wa mahakama. Dhana hiyo pia haitofautiani na kusema kuwa kilichokuwa kinatazamiwa kuwa ni suala lisilotarajiwa kutokwa ,yaani mhusika kufungua madai dhidi ya serikali bila kupitia mfumo wa mahakama, au kutotaka maamuzi yake kwa kina) sasa imekuwa ndiyo kawaida. Kujitoa katika hali hiyo siyo kuikana mahakama bali ni kueleza hitaji la kujitafakari, waangalie kama wanaweza kuoanisha itikadi, matazamio, viwango.

 Kwa jumla katika mazingira kama hayo inabidi muda upite kwanza na licha ya kuwa hivi sasa ni serikali inayoiambia Mahakama ya Afrika ijitafakari imesimama wapi kuhusiana na kanuni za awali za kuanzishwa kwa mahakama hiyo, hali halisi inaweza kuwa tofauti kiasi fulani.

Moja ya sababu zilizofikia mabadiliko katika utendaji wa mahakama hiyo ni kuwa ilikosolewa kwa muda mrefu kuwa haina meno, yaani bila kesi kukubaliwa, kusikilizwa kwanza na nchi mwanachama haipokelewi.

Isitoshe, mwaka 1994 iliundwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuhusu Rwanda, ikifuatia ile nyingine kuhusu Yugoslavia ya zamani, ambako ni mahakama inaunda kesi, si nchi.

Ina maana kuwa kuhitilafiana kati ya kanuni za awali za Mahakama ya Afrika ambayo Tanzania ilisaidia kuundwa kwake na kuwa mwenyejii wake karibu miaka 40 iliyopita ni kielelezo cha historia, kuwa kuna mazingira tofauti wakati ule ukilinganisha na wakati huu.

Hali hiyo inafanya kazi pande zote mbili kwa maana kuwa enzi zile Afrika  ilikuwa inaamini inaweza kuunda chombo cha ngazi ya juu kusaidia kuunganisha Afrika kisheria kuwa na jopo la rufani kwa kesi zinazosikilizwa bila kutengemaa kikamilifu katika nchi wanachama.

Hapakuwa na mazingira ya mahakama za Umoja wa Mataifa zenye madaraka ya kukamata watuhumiwa na kuwafikisha kwa mfano The Hague. Hivi sasa kuna mahakama ya kimataifa ya aina hiyo, wengine wanachota vielelezo vipya huko.

Kwa upande wa pili, enzi hizo mfumo wa vyama vingi ulikuwa bado kwa muongo mmoja, na baada ya hapo ikachukua miaka 20 ya uchaguzi wa kidemokrasia kuona jinsi ufisadi serikalini unavyojenga hema la pamoja na uhuru wa mtu binafsi kwa upande mmoja na uhuru mpana wa bunge na vyama vya siasa.

Habari Kubwa