Bila urafiki na mazingira majanga, maafa hayataisha

10Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bila urafiki na mazingira majanga, maafa hayataisha

KUNA usemi usemao “hakuna lisilowezekana chini ya jua”. Huwa najiuliza chimbuko la usemi huo ni nini? Jibu kamili sina, pengine kilichomanishwa ni kuwa na ari ya kutaka kufanikisha kile cha muhimu katika maisha. Vilevile, ni kama kusema -

Misitu ni rasilimali muhimu kwa vile ndicho chanzo cha mvua, hewa safi na nishati kuni. Bila ulinzi wa misitu kuna hatari ya taifa kugeuka jangwa. PICHA: MTANDAO.

Na Dk Felician B. Kilahama, WCT

-“penye nia pana njia” kwa msingi kwamba ukiwa na uthubutu wa kweli utafanya na kufanikiwa.

Yote heri isipokuwa tujitahidi tukimtanguliza Mwenyezi Mungu au kwa maneno mengine “Mungu Kwanza” kabla ya yote. Hii ni muhimu sana maana yeye ndiye aliyetuumba na binadamu bila kuwapo nguvu ya Mungu au Uwezo wa Kimbingu juu yetu ni sawa na kazibure.

Namshukuru sana Mungu kwa kutofautisha binadamu na viumbe wengine kwanza, kwa kutuumba kwa sura na mfano wake, hii ni heshima kubwa kwetu.

Mungu amewapa wanadamu  uwezo wa  kumiliki na kutawala rasilimali zote duniani isipokuwa kukatazwa kula matunda ya mti uliokuwa katikati ya “Bustani ya Edeni”.

 Hata hivyo binadamu alishindwa kutii amri hiyo na kusababisha udhaifu kwenye kumiliki na kutawala hivyo kupelekea laana kumwandama binadamu mpaka leo.

ATHARI ZA EDENI

Halihalisi tunayoishuhudia nyakati hizi zenye maafa mengi dunia ni matokeo ya udhaifu uliojengeka miaka mingi sana kutokana na kutotii pamoja na kujengeka ubinafsi zaidi kuliko kuwapo mtazamo halisi wa kutumia rasilimali tulizopewa na Mwenyezi Mungu kwa misingi endelevu na kwa faida ya wanajamii wote au kwa maslahi mapana ya taifa letu.

 Kwa hali hiyo shughuli nyingi za kibinadamu mijini na vijijini; zimekuwa na matokeo hasi kwa mazingira.

Mathalani, ukataji ovyo wa miti na ufyekaji wa misitu ya asili bila kufuata kanuni za Uhifadhi wa Mazingira, kuchoma mapori moto au kutotekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini: kumesababisha misitu ya asili na uoto juu ya ardhi kutoweka.

WAKATI WA UHURU

Kabla na baada ya kupata uhuru hali ya mazingira nchini ilikuwa ni ya kijani sana ukilinganisha na ilivyo sasa. Ingawa idadi ya watu ilikuwa chini ya milioni 10 wakati unapatikana na mwaka 1961  sasa inakadiriwa kuwa milioni zaidi ya 55 na mifugo zaidi ya milioni 35; hatuwezi kusema ongezeko hilo ndiyo sababu kubwa ya kupelekea uharibifu wa mazingira kuwa mkubwa kiasi hicho.

Ukweli ni kwamba kushindwa kumiliki na kutawala vyote kwa kutumia njia endelevu. Kukosekana utayari wa kutumia rasilimali asilia ikiwamo misitu; wanyamapori; ardhi, maji, samaki na kadhalika, kwa misingi endelevu.

Ndicho chanzo kikubwa kupelekea maafa kuongezeka. Sasa tunalia na athari za mabadiliko ya tabianchi kumbe kisababishi ni kazi za mikono yetu na kupelekea ongezeko kubwa la joto duniani, matokeo ni maafa kila mahali ikiwemo bara la Afrika kukumbwa na njaa, ukame, mafuriko, kupoteza uhai na mali kama nyumba kubomoka au kuezuliwa paa.

MISITU KUTOWEKA

Uoto wa asili kwenye nchi za Africa ikiwemo Tanzania umetoweka kwa kasi kubwa sana. Tanzania kwa mfano, inakadiriwa kupoteza misitu ya asili kwa kiwango cha hekta kati ya 370,000 na 470,000 kwa mwaka kutegemea hali halisi ya mahalia (locality).

 Hivyo maeneo mengi nchini hayana uoto wa asili kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Kila kukicha uoto wa asili: nyasi, mimea, miti na misitu vinapotea kwa kiwango kikubwa. Ndiyo maana kwa nyakati hizi, tofauti na zamani, mvua ikinyesha baada ya muda mfupi tu mafuriko yanatokea.

Vilevile, msimu wa mvua ukiisha baada ya muda mfupi upatikanaji wa maji unakuwa wa shida (chemichemi zinakauka na mito mingi kuwa na maji kidogo).

Kwa nini kumekuwepo na athari hizo nyakati hizi kuliko zamani?  Binadamu, pamoja na idadi ya watu kuongezeka, hatuishi kirafiki na Mazingira au hatumiliki na kutawala kwa kuzingatia misingi sahihi, na badala yake tumekuwa waharibifu kwa Mazingira na sasa yanatugeuka na kutuangamiza.

Kwa miaka ya nyuma mvua zilikuwa zinanyesha za kutosha nakumbuka nikiwa kijana miaka ya 1950s na 1960s mvua za masika zilikuwa nyingi kiasi cha kushindwa kupata kuni za kupika chakula.

Kaya nyingi zililazimika kuweka kuni za kutosheleza mahitaji nyakati za masika kinyume cha hapo “mtapiga miayo” kutokana na njaa kwa kukosa nishati ya kupikia kisa mvua nyingi wakati wa masika.

Wakati hali ni hivyo mafuriko makubwa au kubomoka madaraja ilikuwa nadra sana tofauti na hali ilivyo sasa. Hali ilikuwa salama zaidi kuliko sasa maana tulikuwa bado tunaishi kirafiki na mazingira hivyo uoto wa asili ulikuwapo wa kutosha.

Kwa maneno mengine, kukiwapo na uoto wa asili wa kutosha  maji ya mvua huingia ardhini taratibu na hatimaye kutiririka kwenye mito hata nyakati za kiangazi lakini pia ardhi au udongo kuhifadhiwa. Hivyo kutokuwapo uoto wa asili wa kutosha kumeleta athari kwa ardhi na upatikanaji maji nyakati za kiangazi ni kubwa sana.

Ongezeko la watu au mifugo kwa mtazamo wangu havijawa tishio kwa maisha yetu na hasa tukizingatia kuwa Tanzania Bara inayo aneo kubwa takribani hekta zaidi ya milioni 88. Kwa idadi ya watu milioni 55 ni sawa na kila mtu kumiliki hekta taribu 1.6 na familia ya watu 10 watakuwa na hekta 16.

 Kwa idadi ya mifugo takribani milioni 35 ni sawa na mtu mmoja kuwa na mfugo mmoja. Hii inaonyesha kuwa kiuhalisia bado ardhi inatosha isipokuwa matumizi yake siyo endelevu.

 Sehemu mbalimbali nchini tunalima kwa kufyeka misitu ya asili (kilimo cha kuhamahama), hatufugi tunachunga mifugo; ardhi inatumika kama haitakiwi kwa vizazi vijavyo.

 Matokeo yake ni kutoweka uoto wa asili na hivyo maji ya mvua kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo. Matokeo yake ni ukame na njaa kutokama na kilimo duni. Maji ya mvua yakishindwa kuingia taratibu ardhini husomba udongo na kila aina ya takataka na kupelekwa mabondeni na kwenye mito.

Hali hiyo inasababisha vina vya mito (riverbeds) kupungua kutokana na kujaa udongo, mchanga, matope na katakataka za kila aina ikiwamo maplastiki. Mfano, Mto Mzimbazi jijini Dar-es-Salaam, umesheheni mchanga na uchafu wa kila aina) hivyo maji ya mvua husambaa haraka na kusababisha mafuriko wakati wa mvua.

Madaraja na barabara kubomoka ni matokeo ya maji ya mvua kutoingia ardhini na badala yake kujaza mito haraka. Isitoshe njia za asili ambazo maji ya mvua hupita zimezibwa hivyo kusababisha maji kuzagaa sehemu ambazo hayastahili kuwapo. Maji yanapokuwa mengi ana nguvu sana na yanapofika kwenye madaraja na kwa sababu kina cha mto kimepungua sana maji hupita kwa shida hivyo kusambaa juu ya daraja na wakati huo yakimomonyoa udongo ulioshikilia nguzo za madaraja hatimaye hubomoka na kusababisha hasara kubwa sana.

ATHARI/KUJIANGAMIZA

Tukubali kuwa sasa hali siyo rafiki maana matokeo ya kutoishi kirafiki na mazingira yanakuwa mwiba kwetu kiasi cha kusababisha madhara makubwa kwa jamii na taifa zima. Tujirudi turekebishe tulikokosea.

Tuzingatie matumizi sahihi ya rasilimali ardhi; tulime kitaalam na kilimo kiwe kijani (green faming), kingo za mito zihifadhiwe na sheria zisimamiwe ipasavyo.

Tuwe wafugaji bora badala ya mazoea ya kuchunga mifugo na tuhakikishe tunazalisha mazao ya kilimo au mifugo kwa tija kubwa kwa kutumia eneo dogo la ardhi. Kwa ufupi: tufanye yote kwa kuzingatia umuhimu wa kuishi kirafiki na mazingira ili tuepuke vifo na kupoteza mali kwa sababu mazingira yakiharibiwa yanalipiza kisasi bila huruma. Tuchukue hatua sasa na kutimiza wajibu wetu ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii huku tukitunza mazingira kwa faida yetu na vizazi vitakavyofuata.

 

Dokta Felician B. Kilahama ni  Mwenyekiti, Taasisi ya Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira (WCST).

Habari Kubwa