Mchungaji Korokoni: Nimevua gwanda la madhabahuni, kumsaka ‘shetani’

12Dec 2019
Sabato Kasika
Serengeti
Nipashe
Mchungaji Korokoni: Nimevua gwanda la madhabahuni, kumsaka ‘shetani’
  • Ukeketaji Wanaofanya kabila lake, ana siri zao kibao
  • Ana maumivu miaka 39 kifo mdogo wake Imani iliyopo ‘Julai marufuku kukeketa’
  • “ Wamekuwa na tabia ya kukeketa kila mwezi Desemba ya mwaka katika kile wanachokitafsiri kiimani ‘mwaka unaogawanyika kwa mbili’ na kuacha ule ‘unaogawanyika kwa saba tu.”

MARA ni mkoa unaotajwa kushika nafasi ya tatu, katika mikoa mitano inayotajwa kuongoza kwa mila potofu za ukeketaji watoto wachanga na wasichana, Serengeti na Tarime.Watangulizi wake Manyara, Dodoma na Singida.

Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly. PICHA : SABATIO KASIKA.

Ziko sababu zinazotajwa kuchangia kuendelea kuwapo vitendo vya ukeketaji, kwenye baadhi ya kabila. Mojawapo ni usiri mkubwa uliopo katika jamii husika zikiamini kukeketa ni sehemu ya mila na desturi zao.

Ni kabila zinazotunza siri za wanaoendeleza vitendo hivyo, ili kuwaepusha wanaokeketa na mkono wa dola. Hali inayosababisha mabinti na kinamama kuendelea kunyanyasika, bila ya kupata msaada.

Inaekezwa kuwapo kabila linaotajwa kuwa kinara wa kuendeleza ukeketaji wilayani Serengeti, licha ya vitendo hivyo kupigwa vita kila kona wanaendeleza, isipokuwa mwezi wa saba ndio hawakeketi wala kufanya sherehe kwa madai ‘una mikosi.’

KULIKONI HIVYO?

Nipashe ilifanya udadisi kwa kumhoji Mchungaji Stephen Korokoni, mkazi wa Mugumu, Serengeti anayetokea katika kabila lililokubuhu kwa tabia hiyo, naye akawa na mengi ya ‘kufunguka.’

Ni ushuhuda aliyoutoa kutoka wenye mahafali ya wasichana wahitimu wa mafunzo ya ujasiriamali katika Nyumba Salama inayohudumia kukwepa ukeketaji, inayomilikiwa na taasisi ya Hope for Girls and Women Tanzania, iliyopo Mugumu, Serengeti.

"Mimi ni mtumishi wa Mungu. Nimefanya kazi ya uchungaji katika Kanisa la...(dhehebu kubwa nchini) kwa zaidi ya miaka 20, kisha nikawa huru ili kupambana na vitendo vya ukatili huu," anasema Korokoni.

Anaeleza sababu ya kujiengua alikokuwa mwaka 1994 hadi 2017 aliporejesha safari ya kuwa nje ya ajira, ili awe huru kwenye kazi ya uchungaji kumudu kupinga vizuri vita dhidi dhidi ya ukeketaji.

"Ninaweza kusema kuwa kwa sasa mimi ni mchungaji huru, ambaye nimejikita zaidi katika kupambana na ukeketaji kuanzia kwenye koo za Wangoreme ninakotokea na nyingine za Wilaya ya Serengeti," anasema.

Anasema, kwa kabila lao (jina tunalo) wamekuwa na tabia ya kukeketa kila mwezi Desemba ya mwaka katika kile wanachokitafsiri kiimani ‘mwaka unaogawanyika kwa mbili’ na kuacha ule ‘unaogawanyika kwa saba tu.”

"Wanakeketa miezi yote isipokuwa wa saba tu. Wanakeketa miaka yote inapokuwa unaoishia na saba mwishoni, pia hawafanyi sherehe yoyote mwezi wa saba wala mwaka unaoshia saba (mfano 2017)," anasema.

Mchungaji Korokoni, anasema ni dai la jamii na wana- imani hao wa ukeketaji kwamba wanaitenga herufi ‘saba’ wakiitafsiri ina mkosi

"Ninaweza kusema kuwa ni mwiko kwa (kabila hilo) kukeketa au kufanya sherehe zozote mwezi wa saba au mwaka unaoishia na saba, lakini miezi mingine na miaka mingine yote, shughuli ni kama kawaida," anasema.

ANAVYOFANYA KAZI

Mchungaji huyo anasema, namna anavyifanya kazi sasa amekuwa wakala wa taasisi ya Hope for Girls and Women Tanzania, katika uhamasishaji jamii kuachana na na ukeketaji wilayani Serengeti.

Anaainisha jukumu lake ni kwamba, anawajibika kuwa mshauri wa mambo ya kiroho, imani na mila za ambazo zinainyanyasa jamii na hasa kinamama, huku haziwaachi salama watoto wa kike.

Anasema, licha ya kuacha jukumu lake la uchungaji kanisani, bado ana heshima hiyo inayosaidia asikilizwe, kuwaondoa wana jamii katika mila potofu.

"Nikuhakikishie kuwa nimesaidia familia yetu kuachana na mila hizo, kwani mimi watoto wangu wote watatu wa kike hawajakeketwa na hata wa ndugu wakiwamo wa dada zangu," anasema Korokoni.

Pamoja na mafanikio hayo, ana kumbukumbu ya majuto ya kufiwa na mdogo wake mwaka 1980, baada ya kukeketwa akiwa amehitimu darasa la saba.

Anasema, ni tukio linalogusa nafsi yake hadi sasa na kumfanya aongeze kasi ya kupambana na ukeketaji hatua aliyoianza muda mrefu, lakini kawa anakutana na vipingamizi kutoka kwenye familia na ukoo.

"Tangu kifo hicho, familia yetu imeachana kabisa na mambo ya ukeketaji, ambao kwa kweli ni mateso makali kwa mtoto wa kike, ambaye anahitaji kusoma kwa ajili ya maisha yake ya baadaye," anasema Mchungaji Korokoni.

Analalamika ukeketaji bado upo katika jamii na kwamba na imefikia kwa watoto wachanga, hivyo anashauri watoto wanapopelekwa hospitali wakaguliwe kama wamekeketwa.

"Daktari akimkagua mtoto na kubaini kuwa amekeketwa, basi mama yake akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili asaidie kuwapata waliofanya unyama huo," anasema.

Mchungaji huyo anasema hilo, akibianisha kugundulika tabia ya watoto wachanga, baada ya kuwapo ufuatiliaji wa serikali na hatua za kisheria.

Pia, anataja mbinu wanazotumia wazazi, wakeketaji na wazee wa mila kuwa ni kuwapeleka watoto porini usiku wa manane wakikwepa kugundulika na kuwafanyia ukatili huo bila huruma.

"Serikali na wadau wengine msichoke kuwafuatilia kwa karibu watu hawa, tuko nyuma yenu ili kukomesha vitendo vya ukeketaji kwa wasichana na watoto wachanga ambao kimsingi ni malaika wa Mungu," anasema.

Kwa mujibu wa sheria za nchi, ukeketaji ni kosa la jinai ambalo mtuhumiwa akitiwa hatiani wanaweza kufungwa hadi miaka 15.

"Kuna madhara mengi kiafya na kisaikolojia yanayosababishwa na ukeketaji kuanzia msihtuko, homa kali, kumwaga damu nyingi na mara nyingine hata kusababisha kifo, kuambukizwa virusi vya Ukimwi," anasema.

Pia, Mchungaji Korokoni, anataja msongo wa mawazo, kuathirika kisaikolojia, ulemavu, kovu la kudumu, maradhi ya fistula, mwanamke kupata shida wakati wa kujifungua na ugumba.

Habari Kubwa