Kili Stars, Zanzibar Heroes msituangushe Cecafa leo

14Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Kili Stars, Zanzibar Heroes msituangushe Cecafa leo

MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa upande wa Kundi B, inatarajiwa kuendela leo kwa kuchezwa mechi mbili za kuhitimisha hatua hiyo ya makundi ambazo zitatoa timu moja itatakayoungana na Kenya kutinga nusu fainali.

Katika michuano hiyo ambayo washindi wawili kutoka katika kila kundi watatinga nusu fainali, Kundi A linaundwa na wenyeji Uganda, Burundi, Eritrea, Somalia na Djibouti wakati Kundi B mbali ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, pia zimo Kenya na Sudan.

Kwa upande wa Kundi A, tayari wenyeji Uganda wameshafuzu na watajua timu itakayoungana nayo kwenda hatua ya nusu fainali baada ya mechi zao za kesho, Jumapili.

Mechi za leo zinatarajiwa kuikutanisha Kilimanjaro Stars yenye alama tatu dhidi ya Sudan ambayo ina pointi moja sawa na Zanzibar Heroes itakayovaana na Kenya yenye pointi sita kileleni mwa Kundi hilo la A.

Hivyo, timu zote tatu, Kilimanjaro Stars, Zanzibar Heroes na Sudan, zina nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Hesabu zinaonyesha endapo Kilimanjaro Stars itaibuka na ushindi dhidi ya Sudan itafikisha alama sita ambazo haziwezi kufikiwa na Zanzibar Heroes hata kama itashinda dhidi ya Kenya leo.

Lakini pia, endapo Kilimanjaro Stars itapoteza na wakati huo huo Kenya ikashinda ama kutoka sare dhidi ya Zanzibar Heroes, moja kwa moja Sudan itafuzu kutokana na kufikisha alama nne hivyo kuipiku miamba hiyo miwili ya Tanzania.

Kwa Zanzibar Heroes nafasi yao ya kufuzu nusu fainali inategemea endapo tu itashinda dhidi ya Kenya kwa idadi kubwa ya mabao huku ikiombea Kilimanjaro Stars itopoteze kwa mabao machache dhidi ya Sudan, hivyo kulingana pointi na Wasudan hao ili linapokuja suala la tofauti nzuri ya mabao, Zanzibar iweze kunufaika.

Ilivyo ni kwamba, endapo Sudan itashinda na wakati huo huo Zanzibar Heroes ikaichapa Kenya, zote zitafikisha alama nne, hivyo timu yenye tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa itafuzu kutokana na miamba hiyo ilipokutana ilitoka sare ya bao 1-1.

Hali hiyo ndiyo inayofanya mechi hizo kuonekana kama fainali, kwani Kenya tu ndiyo itakuwa haina cha kupoteza kutokana na kutaka kulinda heshima leo kwa kushinda mechi zote za hatua ya makundi, wakati zingine zikiwania ushindi ili kuweza kuungana nayo kutinga nusu fainali.

Aidha, kutokana na Kenya kutokuwa na chakupoteza leo kwa kuwa imeshatinga nusu fainali, inaweza kuutumia mchezo huo kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wake ambao walikuwa hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi zilizopita, hivyo kuwa rahisi kwa Zanzibar Heroes kushinda.

Kwa mantiki hiyo, presha kubwa itakuwa kwa Kilimanjaro Stars ambayo inahitaji ushindi wakati huo huo mpinzani wake, Sudan naye akihitaji kushinda ili kutinga nusu fainali.

Hivyo, si mechi rahisi kwa pande zote, lakini Nipashe hatuna shaka yoyote kuelekea mchezo huo kwa kuwa tunaamini kama ambavyo kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alivyoeleza jana kuwa amezifanyia kazi kasoro zilizojitokeza kwenye mechi zilizopita, wachezaji watatekeleza kile walichoelekezwa wakiwa dimbani leo.

Lakini pia, tunazidi kuamini kwamba Mgunda ameisoma vema Sudan baada ya kuishuhudia wakati ikitoka sare dhidi ya Zanzibar Heroes katika mechi yao ya awali, ingawa hilo haliwezi kutufanya kujiaminisha sana kwani hata wapinzani wao watakuwa waliisoma vema ikicheza na ndugu zao wa Zanzibar.

Jukumu letu kama Watanzania ni kuendelea kuelekeza dua zetu kwa Kilimanjaro Stars, lakini pia kwa Zanzibar Heroes ili timu mojawapo iweze kurejea na ubingwa huo nchini, tunaamini wachezaji wataitendea haki dhamana ya kuivaa jezi ya taifa kwa kushinda katika mechi hizo za leo.

Habari Kubwa