Suza yatinga shindano mabadiliko tabianchi

14Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
PEMBA
Nipashe
Suza yatinga shindano mabadiliko tabianchi

CHUO Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA), kimebahatika kuingia kwenye shindano la ‘Mabadiliko ya Tabianchi’ lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa likiwa na lengo la kuleta mabadiliko katika jamii.

Shindano hilo linatarajiwa kufanyika kwa awamu ya kwanza leo (Disemba 14) katika ukumbi wa chuo za SUZA Vuga mjini Unguja.

Akizunguza na waandishi wa habari hizi, Kiongozi wa Serikali ya wanafunzi kutoka Chuo hicho kwa upande wa Pemba, Mohamed Ali Abdi, alisema shindano hilo ni fursa kwao na jamii kwa ujumla.

Alieleza lengo ni kuleta mabadiliko katika jamii ambapo wanafunzi hupewa nafasi ya kutambulisha mawazo yao juu ya jambo fulani ambalo hutangazwa kila mwaka na Umoja wa Mataifa.

“Jambo hilo litasaidia kutoa msaada katika Dunia tutakayoijenga katika miaka ya mbele, shindano hilo linalenga mabadiliko ya tabianchi ambayo ni moja katika ya malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa,” alisema Mohamed.

Alisemaa anaamini shindano hilo litaleta mabadiliko chanya, kwani wataweza kufikisha maoni yao katika Baraza la Umoja wa Mataifa, jambo ambalo ni kuitangaza Zanzibar na kuiletea maendeleo.

“Tunataka tukabiliane na mabadiliko ya tabianchi, kwani imekuwa mbaya sasa, maeneo mengi yameshakumbwa na hali hiyo, hivyo tunaamini kuwa shindano hili litaleta tija kwa jamii yote nzima,” alisema.

Naibu waziri wa Elimu wa Serikali ya wanafuzi wa chuo hicho, Pemba, Mohammed Ali Mohammed, alieleza kuwa shindano hilo litawanufaisha sana kwani watapata uzoefu, kujitolea, kujiamini na kuelewa kwa upana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na namna ya kukabiliana nayo.

“Tunaomba wananchi washiriki katika shindano hilo na watoe mawazo yao, yatakayowajengea uwezo zaidi kwa kile watakachokwenda kukieleza nje ya nchi, kwani mabadiliko ya tabianchi yanaathiri siku hadi siku duniani kote,” alieleza.

Nae, Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa Mataifa kupitia SUZA Pemba, Abdul-latif Soud Mussa, alisema ipo haja kwa vijana kushiriki katika shindano hilo la ili kuleta mabadiliko chanya kwa jamii.

Habari Kubwa