Mamilioni wenye vitambulisho Nida hawajasajili laini kwa alama vidole

14Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mamilioni wenye vitambulisho Nida hawajasajili laini kwa alama vidole

ZIKIWA zimebaki siku 17 kabla ya kuzimwa laini zote za simu ambazo hazijasaliwa kwa mfumo wa kieletroniki, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imebaini watu milioni tatu wana namba za utambulisho wa uraia, lakini hawajajisajili.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hali ya usajili na vikwazo vyake.

Alisema katika watu hao milioni tatu wenye namba za vitambulisho, wanatarajiwa kusajili laini milioni 5.6 kwa kuwa mtu mmoja anamiliki laini zaidi ya moja.

“Laini zilizosajiliwa kwa ujumla ni 47,063,603 hadi kufika Desemba 10, mwaka huu, ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1.

"Idadi ya laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole ni 19,681,06 sawa na asilimia 42 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 7.6,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema idadi ya watu wenye namba za usajili, lakini hawajajitokeza kujisajili, inatokana na kukosa uelewa wa kutosha wa namna ya kujisajili na namna ya kutambua namba za vitambulisho vyao.

Aliwataka Watanzania waliojisajili kwa alama za vidole, lakini hawajapewa vitambulisho, kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda 15096 na kuandika jila kwanza, jina la mwisho, tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa, jina la kwanza la mama na jina la mwisho la mama ili kupata namba ya usajili kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Alisema njia ya pili ya kutumia ili kufahamu namba hizo ni kupiga *152*00# kisha kuchagua namba 3 (ajira na utambuzi).

Kilaba alisema njia ya tatu ni kutumia anuani ya https://services.nida.go.tz/nidaportal/get_nin.aspx kupata namba ya usajili kutoka Nida.

“Kila Mtanzania aliyejisajili anapaswa kutumia njia hizi ili kupata namba yake ya usajili na kwenda kusajili laini zake na kama atakutana na matatizo kadhaa, basi anapaswa kufuata maelekezo ikiwamo ya kukumbuka jina la mzazi na namba aliyojisailia Nida,” alisema Kilaba.

Aprili 26, mwaka huu, Rais John Magufuli, akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Mbeya, aliitaka TCRA kuanza usajili kwa mfumo wa kieletroniki ili kuwalinda watumiaji dhidi ya matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano ya simu nchini.

Alisema lengo ni kuwawezesha watumiaji kutambuliwa kama wanatumia huduma za kuongeza thamani kama vile huduma za benki kupitia simu za mkononi, uhamisho wa fedha kwa njia ya simu za mkononi, malipo ya kitamtandao kwa huduma kama za umeme, maji na ada za shule.

Dhumuni lingine ni kuimarisha usalama wa watumiaji na kuwezesha waendeshaji wa mtandao kuwahudumia wateja wao kwa usalama.

Mei Mosi, mwaka huu, TCRA walianza rasmi kazi ya usajili kwa alama za vidole kwa kushirikiana na kampuni za simu za mikononi na kazi hiyo itafungwa rasmi Desemba 31, mwaka huu saa 6:00 usiku na mtumiaji wa simu ambaye hatajisajili laini yake, itakuwa imefungwa rasmi.

Habari Kubwa