Upendeleo miradi wamchefua DC

14Dec 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Upendeleo miradi wamchefua DC

UPENDELEO wa uwekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika ukanda wa milimani wilayani Hai, umemchefua Mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya na kuagiza kuanzia sasa huduma kama afya, barabara na elimu kuelekezwa ukanda wa chini wa tambarare.

Ole Sabaya aliagiza jana kumalizwa kwa malalamiko hayo ya wananchi wa tambarare, alipozindua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Heshima cha Longoi kinachojengwa katika Kata ya Weruweru.

"Nimesikia malalamiko yenu kwamba kila mradi ukija unaelekezwa ukanda wa milimani (Machame na Masama) na nyie hata barabara hazipitiki.

"Najua kuna kinamama wajawazito wanateseka kupita lile daraja la Mnepo kuja Kwa Sadala hadi Hospitali ya Wilaya. Mkurugenzi Mtendaji (Yohana Sintoo) naomba tatizo hili ulimalize na yasijitokeze tena malalamiko haya, ndiyo maana leo (jana) tumewaletea kituo hiki cha afya cha heshima kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais John Magufuli," alisema.

Kituo hicho kitahudumia zaidi ya wananchi 19,000 wa kata tatu za Weruweru, Masama Rundugai na Mnadani.

Kwa miaka 58, sasa wananchi hao wamekosa huduma za afya na kulazimika kuzifuata umbali wa zaidi ya kilomita 20.

"Maeneo haya ya tambarare yamekuwa yakionekana kama yametengwa na kubaguliwa huku maeneo ya juu milimani yakionekana kuwa na maendeleo ikiwamo kuwa na huduma zote muhimu za kijamii.

"Baada ya kuona dhana hiyo iliyojengeka kwenu, nilibuni namna ya kuwasaidia kwa kufanya jitihada za kutafuta fedha ili kujengwa kwa kituo hiki ambacho kinatarajiwa kuhudumia maelfu ya wananchi wa maeneo haya ya tambarare," alisema.

Akizungumza wakati akizindua ujenzi huo, Ole Sabaya alisema kituo hicho kitagharimu zaidi ya Sh. milioni 300, fedha ambazo zinatokana na michango kutoka katika vyama vya ushirika.

"Fedha hizi zimetolewa na vyama vya ushirika, tuliwaomba katika bajeti yao ya mwaka 2018/2019 kutenga asilimia 50 kwa ajili ya kuchangia ujenzi huu, lakini pia pamoja na hilo bado wananchi mnapaswa kushiriki kutoa mchango wenu wa nguvu kazi na fedha," alisema.

Alitoa onyo kwa wananchi wenye tabia za wizi wa vifaa vya ujenzi kwamba yeyote atakayebainika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Akizungumzia ujenzi wa kituo hicho, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk. Irene Haule, alisema kituo hicho kitakamilika baada ya miezi mitatu na kwamba watatumia mafundi jamii ili kupunguza gharama za ujenzi.

"Kituo kitakuwa na majengo matatu ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje, jengo la mama na mtoto pamoja na jengo la maabara na kitakamilika ndani ya miezi mitatu kwa kutumia fedha hizo," alisema.

Akizungumzia hali upatikanaji wa huduma za afya katika wilaya hiyo, Dk. Haule alisema kuna upungufu wa vituo vya afya kwa zaidi ya asilimia 65 na kwamba ujenzi huo utasaidia kupunguza tatizo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo, aliwataka wananchi kutoiba au kuhujumu miundombinu ya mradi huo.

Mwenyekiti wa Bodi za Vyama vya Ushirika wilayani Hai, Fredrick Urassa, alisema vyama vya ushirika vilikubali wito wa kuchangia ujenzi wa kituo hicho kutokana na ukweli kwamba hapo awali vyama hivyo vilikuwa vikijikita katika kutoa maendeleo katika jamii, lakini dhana hiyo ilikufa baada ya ubadhirifu kushika kasi katika ushirika.

Habari Kubwa