Waziri aagiza mhandisi akamatwe

14Dec 2019
Nebart Msokwa
Nipashe
Waziri aagiza mhandisi akamatwe

WAZIRI wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, ameliagiza Jeshi la Polisi kumkamata na kumsweka ndani Alistides Kanyomo, mhandisi wa Kampuni ya Mbesso Construction Ltd ya jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni tatu za mradi wa maji katika Bonde la Mwakaleli wilayani Rungwe.

Alitoa agizo hilo juzi alipotembelea mradi huo ulioanza miaka 11 iliyopita, lakini mpaka sasa haujakamilika na hivyo kusababisha wananchi katika vijiji 18 vya Halmashauri za Busokelo na Rungwe kukosa maji.

Alisema baada ya kupitia mpango kazi wa mradi huo, amebaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za mradi, hali ambayo alidai serikali haiwezi kuvumilia.

Waziri huyo alisema katika mpango kazi huo, ameona andiko linaloonyesha kuwa ofisi ya muda ya kampuni hiyo iliyojengwa kwenye eneo la mradi imegharimu Sh. milioni 100, lakini alipofika kuikagua, akabaini ni kibanda kidogo cha mabati ambacho hakiwezi kugharimu hata Sh. milioni moja.

“Wamelipwa Sh. bilioni tatu mpaka hivi sasa, lakini hakuna ambacho kimeshafanyika, hapa ninaona kuna kibanda wamejenga kwamba ni ofisi zao za muda, wanadai wamekijenga kwa Sh. milioni 100 wakati ni cha mabati kuanzia chini mpaka juu," alilalama.

Alisema serikali haiwezi kuvumilia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi zikichezewa kwa kiwango hicho, hivyo akaagiza askari polisi kumkamata msimamizi wa mradi huo, Kanyomo na kumweka ndani ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha hizo.

“Naagiza mkamateni mhandisi anayesimamia mradi huu bila kujali kama ndiye mmiliki wa kampuni au la, mwekeni ndani ili tuchunguze kwanza matumizi ya fedha zilizotumika kama zinaendana na kazi iliyofanyika," aliagiza.

Prof. Mbarawa pia aliiagiza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mbeya (Mbeya-WSSA) kuvunja mkataba na mkandarasi huyo mara moja ili mradi huo usimamiwe moja kwa moja na serikali kupitia mamlaka hiyo ili kuhakikisha mradi huo unakamilika na wananchi hao wanapata maji haraka.

Awali, Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete, alidai wananchi wa Mwakaleli wanapata shida ya upatikanaji wa maji, hivyo akaiomba serikali kusimamia yenyewe mradi huo ili kuhakikisha wananchi hao wanapata maji.

Alisema mradi huo umechukua muda mrefu kiasi kwamba wananchi wameanza kupoteza imani na serikali kutokana na kukosa huduma ya maji.

“Mradi huu ulianza tangu mwaka 2008 na sasa ni mwaka 2019, umechukua miaka 11 bila kukamilika, wananchi wetu wameanza kukata tamaa, hivyo nakuomba waziri uwaondoe hawa makandarasi na badala yake mradi huu usimamiwe moja kwa moja na serikali ili wananchi wangu wapate maji,” aliomba.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya, alisema alipoingia wilayani Rungwe mwaka 2016, alikuta miradi miwili ya Masoko na Mwakaleli ikiwa na matatizo makubwa na kwa kushirikiana na Wizara ya Maji waliamua kuanza kushughulikia mradi mmoja mmoja ili kumaliza matatizo yaliyokuwapo.

Alisema walianza na mradi wa Masoko ambao kwa sasa unaendelea vizuri na sasa wameamua kugeukia mradi huo wa Mwakaleli ili kutatua matatizo yake na kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanapata maji safi na salama.

Habari Kubwa