Daktari kizimbani tuhuma kuomba rushwa ya ngono

14Dec 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Daktari kizimbani tuhuma kuomba rushwa ya ngono

DAKTARI Massoud Suleiman Abdallah, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Chake Chake, Pemba, akikabiliwa na mashtaka ya kumuomba rushwa ya ngono mgonjwa.

Daktari huyo anatuhumiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mgonjwa ambaye ni mama mjauzito aliyefika Hospitali ya Chake Chake kwa ajili ya matibabu.

Baada ya mtuhumiwa huyo kupanda kizimbani, alisomewa shitaka lake na mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Ramadhan Suleiman Ramadhan.

Mwendesha Mashtaka huyo alidai mtuhumiwa alitenda makosa mawili, la kwanza likiwa la Novemba 21, mwaka huu majira ya kati ya saa 3:55 na saa 4:00 asubuhi, katika Hospitali ya Chake Chake, aliomba rushwa ya ngono kwa mgonjwa aliyekwenda hospitalini hapo kwa ajili huduma ya uchunguzi ya ultra sound.

Alidai kitendo hicho ni kosa kisheria kwa kuwa ni kinyume cha Kifungu cha 58 cha Sheria ya Rushwa Na. 1 ya Mwaka 2019 ya sheria za Zanzibar.

Alidai kosa la pili lilifanyika siku hiyo hiyo, kwamba mtuhumiwa akiwa mwajiriwa wa serikali katika Wizara ya Afya, alitumia nafasi yake vibaya kwa kutaka kufanya ngono na mgonjwa aliyefika hospitali kwa ajili ya matibabu.

Alidai kufanya hivyo ni kosa kisheria kwa kuwa ni kinyume cha Kifungu cha 53 na 61 cha Sheria Na. 1 ya Mwaka 2012 ya sheria za Zanzibar.

Mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo na kuiomba mahakama impatie dhamana kupitia mawakili wake, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama kwa masharti ya wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa serikali na kutia saini bondi ya Sh. milioni mbili.

Mshitakiwa alitimiza masharti na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani huko Febuari 27, mwakani.

Novemba 21, mwaka huu, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca) kisiwani Pemba, ilimkamata daktari huyo akituhumiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mgonjwa wake kama malipo ya huduma ya uchunguzi ya ultra sound.

Habari Kubwa