JPM kuongoza mapokezi ndege iliyokamatwa leo

14Dec 2019
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
JPM kuongoza mapokezi ndege iliyokamatwa leo

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuongoza wananchi mkoani Mwanza kupokea ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imekamatwa Canada.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema ndege hiyo itapokewa katika jengo jipya la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Alisema Rais Magufuli ataongoza wananchi watakaojitokeza katika mapokezi ya ndege hiyo.

'Ile ndege yetu iliyokuwa imekamatwa kule Canada, sasa imeachiwa. Kwa furaha sana, kwa niaba ya wana Mwanza kesho (leo), Mheshimiwa Rais pale uwanja wa ndege jengo jipya, atatuongoza kupokea ndege yetu, ambayo imenunuliwa kwa fedha za Watanzania.

"Nimekuja hapa kuwatangazia wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi, kuanzia saa nane kamili geti litakuwa wazi, hata kabla ya hapo mpaka saa 10 atakapokuja Rais, tujitokeze kwa wingi kuunga mkono juhudi za Rais," aliomba.

Novemba 23, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, alitangaza kushikiliwa kwa ndege hiyo Canada.

Prof. Kabudi alidai kumekuwa na hujuma kubwa zinazofanywa na mabeberu kwa lengo la kurudisha nyuma juhudi na maendeleo ya nchi.

Alisema mara baada ya ndege hiyo kukamatwa, alimwita Balozi wa Canada nchini na kumweleza namna Serikali ya Tanzania inavyokasirishwa na vitendo vya ndege zake kukamatwa nchini humo kila ikifikia hatua ya kurudi Tanzania.

“Limetokea jambo la kusikitisha ambalo ni vyema Watanzania pia walielewe jinsi ambavyo hujuma za kibeberu zinafanyika kurudisha kasi ya maendeleo, tena kwa mara ya tatu ndege ambayo ilitakiwa kufika Tanzania, imekamatwa tena Canada na kesi ipo mahakamani.

“Aliyefanya hivyo ni mtu yuleyule aliyekamata ndege yetu Afrika Kusini, tukaenda mahakamani tukamshinda, sasa amekimbilia Canada na amekamata ndege yetu ya Bombadier Q400," alisema.

Habari Kubwa