Membe, Kinana, Makamba kikaangoni

14Dec 2019
Romana Mallya
Nipashe
Membe, Kinana, Makamba kikaangoni

HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeazimia wanachama wake watatu, Abdulrahman Kinana, YuSsuf Makamba na Bernard Membe, waitwe na Kamati ya Usalama na Maadili ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili.

Wakati vigogo hao wakiwekwa kikaangoni, NEC imewasamehe na kutoa tahadhari kwa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Maazimio hayo yametokana na kikao chake kilichofanyika jana jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, NEC imeamua Mzee Makamba, Membe na Kinana waitwe na kuhojiwa na kamati hiyo kujibu tuhuma zao kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Kanuni za Maadili na Uongozi.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho kilipokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja taarifa ya Kamati Kuu kuhusu uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM wa kuwasamehe wanachama walioomba radhi kwake.

“Walioomba radhi kwake ni January Makamba, Nape na Ngeleja baada ya kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, kikao hicho kimewataka wanachama hao kujirekebisha na kutorudia makosa yao la sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama ikiwamo kufukuzwa uanachama.

WATEULIWA KUGOMBEA

Taarifa hiyo ilisema awali Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa majina ya wagombea wa nafasi za uongozi katika chama na jumuia.

“Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha ni Dk. Batilda Buriani, Zelothe Stephen na Bakari Msangi. Wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Iringa ni Mafanikio Kinemelo, Hilary Kipingi na Lucas Lwimbo,”ilitaja.

Kwa upande wa wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mtwara, taarifa hiyo iliwataja waliopitishwa kuwa ni Petro Mwendo, Mustafa Mohamed na Selemani Sankwa na wakati wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Dodoma ni Damas Kasheegu, Baraka Mkunda na Christopher Mullemwah.

“Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Pwani ni Mary Joseph, Fredrick Makachila na Samaha Said,” ilieleza taarifa hiyo.

MSIMAMO WA JPM

Katika kikao hicho, taarifa ilieleza kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli, amesisitiza kazi ya urais ni ngumu na ataheshimu utamaduni na desturi za CCM, Kanuni, Katiba ya CCM na Katiba ya nchi.

Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa hiyo, alisema CCM ni kiwanda cha kuzalisha viongozi na kwa utaratibu ambao chama kimejiwekea kitampata mtu bora zaidi atakayepokea uongozi baada yake.

“Nawashukuru sana viongozi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chetu kwa kuzisimamia vizuri serikali zetu mbili, hivyo kuwezesha kupatikana mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.

“Tukaendelee kujenga umoja, kuimarisha ujenzi wa chama na tunapoelekea katika chaguzi zinazokuja tukaepuke makundi na tuendelee kuisimamia serikali ikiwamo kukagua miradi ya kimaendeleo katika maeneo yetu,” alisema Rais Magufuli.

Habari Kubwa