Dante, Tariq sasa wainogesha Yanga

14Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Dante, Tariq sasa wainogesha Yanga

YANGA imeanza kunoga 'mdogomdogo' baada ya kujiimarisha kwa kumsajili mshambuliaji chipukizi Mtanzania Tariq Seif, aliyejiunga na klabu hiyo akitokea nchini Misri alipokuwa anacheza soka la kulipwa huku ikifanikiwa kumrejesha kikosini beki wao kisiki, Andrew Vincent ‘Dante’.

Tariq aliyekuwa anachezea klabu ya Dekernes FC ya Daraja la Pili nchini Misri ambayo alijiunga nayo msimu huu akitokea Biashara United ya Mara, aliwasili juzi jijini Dar es Salaam na kupokewa na Katibu Mkuu wa Yanga, David Ruhago kabla ya jana Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla kumtambulisha rasmi kupitia ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo, Tariq ambaye msimu uliopita aliitungua Yanga katika mechi ya Ligi Kuu wakati akiichezea Biashara United, anaelezwa kulazimika kurejea nchini ili kunusuru kiwango chake kutokana na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Dekernes FC.

Kabla ya kutua Biashara United, Tariq anayetarajiwa kuwa pacha wa David Molinga dimbani baada ya Mnamibia Sadney Urikhob na Mganda Juma Balinya kuachana na klabu hiyo, alianzia soka lake katika Klabu ya Transcamp kisha Mbao FC.

Katika hatua nyingine, kurejea kwa Dante katika kikosi cha Yanga kumetokana na klabu hiyo kushinda rufaa dhidi ya beki huyo baada ya kukata rufaa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Yanga walimkatia mchezaji huyo rufaa hiyo TFF baada ya Dante kugoma kurejea kikosini akishinikiza alipwe kwanza stahiki zake mbalimbali, ikiwamo fedha za usajili.

Na jana uongozi wa Yanga, ulisema: “Uongozi wa mabingwa wa kihistoria Tanzania, (Yanga SC) unamkaribisha tena kikosini beki @vicentandrew ‘Dante’ baada ya kumalizika kwa shauri la kesi baina ya pande mbili.”

Habari Kubwa