Klabu zitangulize maslahi ya wachezaji dirisha dogo

16Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Klabu zitangulize maslahi ya wachezaji dirisha dogo

HATIMAYE dirisha dogo la usajili kwa klabu za Tanzania Bara kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao, limefunguliwa rasmi leo kabla ya kufungwa ifikapo Januari 15, mwakani.

Kufunguliwa kwa dirisha hilo ni nafasi pekee kwa klabu hususan za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza kuboresha idara ambazo zilikuwa zimepwaya ama kuandamwa na majeruhi.

Tayari baadhi ya klabu tangu wiki iliyopita zilianza kutiliana saini mikataba na wachezaji wapya inaowataka kabla ya dirisha hilo kufunguliwa leo, lakini pia zikitangaza kuvunja mikataba na nyota wao wengine.

Tunatambua katika dirisha hili kama lilivyo lile kubwa, pia wapo wachezaji ambao watatemwa ili kutoa nafasi kwa nyota wapya ambao klabu husika zinaamini wanaweza kuzisaidia kutimiza malengo yao. 

Hata hivyo, kutemwa huko hakuwezi kuwa safari ya mwisho kwao kisoka kwani upo msemo wa wahenga usemao "ukisema wa nini, wenzako wanajiuliza watampata lini".

Katika hilo, tunaushahidi wa kutosha kwa baadhi ya wachezaji ambao wamewahi kuonekana hawafai na kutemwa, lakini baada ya kwenda kwingineko wakang'ara na baadaye kusajiliwa tena na klabu zilizowatema awali. 

Kwa mantiki hiyo, wachezaji watakaotemwa hawana budi kutambua hayo ndiyo maisha ya soka na kinachotakiwa ni kupambana zaidi kwa klabu zitakazowasajili ili kuthibitisha ubora wao. 

Aidha, tunafahamu wazi zipo klabu ambazo zimetega mitego yao zikisubiri wachezaji watakaotemwa hususan kutoka kwa klabu kubwa ili ziwasajili. Katika hilo, Nipashe tungependa kuona klabu zikitangulia kwanza kutangaza wachezaji zinaowatema kabla ya kuanza kusajili wapya ili kuwapa fursa ya kujiweka sokoni mapema.

Hatutarajii kuona wachezaji wakutemwa katika dirisha hili wakiwa wa mwisho kutangazwa baada ya klabu husika kufanya usajili kwa kuwa kufanya hivyo si kuwatendea haki.

Lakini ni wakati wa wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi katika vikosi vya kwanza kuomba kuondolewa ili kuokoa viwango vyao na vipaji kwa ujumla. 

Tunatambua wapo wachezaji ambao walishawishika kusajiliwa na baadhi ya klabu kutokana tu na fedha ama ukubwa wa klabu na baadaye kujikuta wakisugua benchi katika kila mechi ama kuishia kupata nafasi chache dimbani wakitokea benchini. 

Hivyo, wachezaji kama hawa, hawana budi kuomba kuondoka ama kutolewa kwa mkopo badala ya kuendelea kusugua benchi ama kusubiri kucheza wakitokea benchini.

Kwa maana hiyo hatutarajii kuona kunakuwa na klabu zitakazowabania wachezaji ambao hawapati nafasi kuondoka ama kuwatoa kwa mkopo kama wanamalengo nao kwa baadaye.

Tunayasema hayo kutokana na kutambua kuwa soka kwa sasa ni biashara na kwa wachezaji hiyo ni sehemu ya maisha na ndiyo kila kitu kwao katika kuendesha maisha ya kila siku.

Hivyo, tunatarajia kuona usajili wa dirisha hili kanuni na sheria zikifuatwa, lakini kwa klabu zikitanguliza mbele maslahi ya wachezaji wao kwa kuwasikiliza maoni yao hususan wale wasiopata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Habari Kubwa