Kituo cha mabasi kuwa cha kimataifa

23Dec 2019
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Kituo cha mabasi kuwa cha kimataifa

MRADI wa ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi mkoani Dodoma utakapokamilika utakuwa na  huduma kama zilizopo kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Mohammedi Builders Ltd, Mohammedi Jafrej, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea mradi huo wa kituo cha mabasi uliopo eneo la Nzuguni jijini hapa.

Jafrej alisema mradi huo utakapokamili utakuwa na huduma za kisasa mfano wa huduma za viwanja vya ndege kutokana na uwepo wa maeneo maalumu ya huduma kwa abiria na wananchi wengine.

Alisema kituo hicho tofauti na vingine kitakuwa na eneo maalumu la VIP, ambalo litakuwa na huduma zote hapo bila kuingiliana na watu wengine wanaotumia kituo hicho.

Aliongeza kuwa kutakuwa na kumbi kubwa tatu zenye huduma zote ndani bila kuingiliana zitakazotumika kwa abiria wengine na wananchi wakisubiri usafiri au wageni wao.

Pia alisema eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuingiza mabasi zaidi ya 300, kwa wakati mmoja pamoja na eneo la maegesho  ya magari mengine ndani  na nje ya kituo hicho.

Kuhusu ujenzi wa kituo hicho, alisema ulitarajiwa kukamilika Desemba 2019, lakini kutokana na kuongezewa eneo la ujenzi unatarajiwa kukamilika Februari 2020.

Alitaja baadhi ya maeneo yaliyoongezwa kwenye mkataba ni miundombinu ya barabara ndani na nje ya kituo hicho ambayo itatumika kwa ajili ya kuingia na kutoka.

Jafrej alibainisha maeneo mengine waliyoongezewa katika mkataba ni pamoja na maegesho ya magari ndani ya kituo hicho na wanaendelea na ujenzi ili kukamilisha ndani ya wakati.

Daudi Ezekiel, mkazi wa Nzuguni aliomba mradi huo utakapokamilika kuwekwe mikakati ya kutunzwa  ili kutumika kwa malengo na mipango  iliyopangwa ndani ya kituo hicho.

Aliuomba uongozi wa jiji kuweka mikakati ya wafanyabiashara ndogondogo pamoja na wajasiriamali wengine ili kuepuka vurugu ndani ya kituo hicho.

 “Tunaomba kituo kitakapokamilika pawepo watu maalumu getini kwa ajili ya kuwasaidia wasiojua eneo la kupata huduma husika, nasikia kutakuwa na hoteli kubwa humo ndani na huduma zingine nadhani si kila atakayefika hapo atahitaji kusafiri wengine watakwenda kupata huduma,” alisema.

Habari Kubwa