Mabadiliko Katiba TFF yachochee maendeleo

23Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Mabadiliko Katiba TFF yachochee maendeleo

MKUTANO Mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umefanyika mwishoni mwa wiki na moja ya ajenda ya mkutano huo ilikuwa ni kubadilisha baadhi ya vipengele vya katiba ya shirikisho hilo ambavyo vilipita kwa asilimia 100.

Mabadiliko hayo yamefanyika kwa kufuata mwongozo kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) pamoja na la Afrika (Caf), kama ambavyo vyama vingine vya soka barani Afrika vilivyotekeleza maelekezo kutoka kwa wasimamizi hao wa ngazi za juu kabisa kwenye mchezo wa kandanda Afrika na duniani.

Katiba ndio msingi wa kila jambo, hivyo hili limepita na kilichobakia ni kutekeleza matakwa yaliyomo kwenye katiba hiyo mpya ambayo kiuhalisia yatakwenda hadi kwenye ngazi za mikoa.

Hata hivyo, kipengele ambacho kilionekana kuleta mjadala mkubwa miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo mkuu ni idadi ya wapiga kura kupungua, hasa kukizingatiwa kuwa awali kila mkoa uliwakilishwa na wajumbe wanne, lakini katiba mpya inasema wapigakura sasa watakuwa wawili kutoka kila mkoa.

Kipengele hiki kimesumbua na kuleta changamoto kwa wajumbe, lakini mwisho wa siku ibara hiyo ilibadilishwa na hatimaye sasa mkutano mkuu wa TFF utakuwa unahudhuriwa na wajumbe 87 badala ya awali ambao walikuwa ni zaidi ya 137.

Baada ya wajumbe kupitisha katiba mpya na kusajiliwa, viongozi wapya watakaoingia katika mkutano mkuu watakuwa ni wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa mkutano mkuu, huku ikielezwa kwa "mdomo" kuwa siku za usoni, makatibu ambao sasa watakuwa wasimamizi wa vituo, wataajiriwa ili kufanya watumie muda mwingi kufanya kazi za maendeleo ya soka mikoani mwao.

Nipashe inaamini kuwa mabadiliko yoyote yanayofanywa na Fifa, Caf na TFF yanalenga kuimarisha na kuukuza mchezo wa soka ambao unapendwa na mashabiki wengi zaidi duniani, hivyo wadau wote wanapaswa kuhakikisha hakuna kinachokwamisha katika kufikia maendeleo.

Hatuamini hata siku moja viongozi wakuu watakubali kufanya mabadiliko ambayo yatarudisha nyuma maendeleo ya soka na hivyo kuondoa ushindani na burudani ambavyo mashabiki wake husubiri kila wanapokuwa viwanjani au mbele ya televisheni (nyumbani au vibanda umiza).

Tunashauri kuwa katiba imeshapitishwa hivyo kinachohitajika ni utekelezaji sasa, na pia ni wakati wa kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo ya mikoa yote ya hapa nchini na kwa kufanya hivyo, TFF itakuwa na kazi nyepesi ya kuunganisha nguvu za wanachama.

Lengo letu ni kuona soka linapiga hatua kutoka hapa tulipo kwa klabu zetu kutisha katika michuano ya kimataifa jambo ambalo litasaidia wachezaji wanapoitwa timu za taifa kuwa msaada mkubwa na hatimaye kuweza kuiletea nchi yetu sifa kwa kutwaa mataji, na hilo litawezekana tu kama mabadiliko haya yatafuatwa bila kupepesa macho.

Itakuwa ni jambo la kushangaza kama viongozi wa mikoa wataacha kuangalia majukumu yao ya msingi ya kuendeleza soka ili klabu na timu zao za mikoa ziweze kufanya vema katika mashindano mbalimbali, hatimaye kuwa msaada kwa timu za taifa, na badala yake kuhamishia nguvu kwenye kuwania nafasi za uchaguzi pekee.

Tunawakumbusha kuwa huu ni wakati wa kuweka mbele maslahi ya soka na kusahau maslahi binafsi ambayo kama wadau watayapa kipaumbele, mikoa na baadhi ya klabu zitaendelea kuwa wasindikizaji kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki ndani na nje ya Tanzania.

Kama mataifa mengine yamekubali kufanya mabadiliko haya, Tanzania pia tunatakiwa tuchukulie kuwa ni jambo la kawaida kwa sababu tunaamini hakuna suala ambalo litapitishwa na lisiwe na malengo ya kuleta mafanikio.

Habari Kubwa