Karia na mzigo mzito Cecafa kuliko wa TFF

23Dec 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Karia na mzigo mzito Cecafa kuliko wa TFF

TANZANIA imepata bahati nyingine kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, baada ya Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia, kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Nichukue fursa hii kumpongeza Karia na Watanzania wote kwa dhamana hii ya miaka minne.

Ninatambua kama Karia ni kiongozi ambaye tangu aanze kuiongoza (TFF), soka la Tanzania siyo kama limekua sana, lakini limeonekana kuanza kutoka shimoni na kuelekea ambako Wabongo walikuwa wanataka lielekee.

Kwa maana hiyo huenda kile alichokileta TFF au bahati aliyokuwa nayo tangu atue huko, inaweza pia kuifanya Cecafa nayo kuinuka.

Kwa sasa Cecafa iko hoi bin-taaban. Ni shirikisho kongwe kabisa Afrika, lakini kwa sasa linapitwa hadi na Cosafa ambalo lilikuja kwenye miaka ya karibuni, nchi za Kusini mwa Afrika zote zilipopata uhuru, sasa zinainyang'anya Cecafa baadhi ya wanachama wake, nchi za Malawi, Zimbabwe na Zambia ambazo zilikuwa zinacheza michuano ya Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame) na Kombe la Chalenji, wakati huo ikiwa na msisimko wa aina yake.

Pamoja na kwamba kuna baadhi ya watu wamekuwa wakimsema sana Katibu Mkuu, Nicolaus Musonye kuwa ni mmoja wa watu ambao wamesababisha Cecafa kudumaa, lakini pia akikaa madarakani kwa zaidi ya miaka 25, binafsi pamoja na mapungufu aliyokuwa nayo, nampongeza kutokana na uvumilivu alionao, kiasi cha kuifikisha hata hapa ilipo.

Tatizo la Cecafa wala si Musonye, bali kuna matatizo mengi mtambuka ambayo yakifanyiwa kazi yanaweza kurekebishika.

Utawala wa Musonye, hadi anatangaza kuondoka mwakani, bado anaiachia Cecafa ikiwa na mdhamini ambaye anatoa zawadi kwa mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu kwa miaka mingi sasa. Naye ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Ni wajibu wa Karia na safu mpya ya uongozi kukaa na Rais huyo, kumwomba aendelee na udhamini wake ambao ndiyo unaofanya michuano hiyo iendelee kuwapo, ikiwezekana hata kama kuna kidogo cha kuongeza basi aongeze, na Musonye ataendelea kukumbukwa kwa hilo.

Pia Karia anatakiwa alete vitu vingine vipya ambavyo vitafanya michuano hiyo kuwa bora zaidi kama vile mfumo mpya, pamoja na wadhamini.

Sidhani kama kitengo cha masoko kikifanya kazi yake sawa sawa kwenye nchi zote za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinaweza kukosa wadhamini walau watatu au wanne ili kuboresha michuano hiyo.

Pia mfumo wa Kombe la Kagame na Chalenji uangaliwe upya kuanzia kipindi cha ratiba, kutoka kuwa ya kituo kimoja hadi kuwa ya nyumbani na ugenini.

Karia aangalie kuwapo na uwezekano wa kuchezwa kwa hatua ya mtoano nyumbani na ugenini na kubakisha timu nane ambazo zinapangwa makundi mawili ambazo nazo zicheze kwa mtindo wa nyumbani na ugenini kutafuta timu mbili za juu zitakazokwenda kucheza nusu fainali na fainali.

Na ratiba ya michuano hii iwe kwenye muda wa Kalenda ya Fifa, klabu zinapokuwa kwenye mapumziko kupisha mechi za kimataifa. Haijalishi hata kama ikiwa ni kwa mwaka mzima, lakini unapopatikana mwanya wa tarehe za Fifa, basi mechi zichezwe.

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo Karia anatakiwa ayaangalie kwa macho mawili ili kuitoa Cecafa hapa ilipo na kuipeleka mbele badala ya kuendelea kuiendesha kwa kukariri. Hongera Karia, lakini Cecafa ni mzigo mzito zaidi ya TFF, kwa sababu inahitaji mabadiliko makubwa.

Habari Kubwa