Usafiri mabasi bado shida Ubungo

24Dec 2019
Maulid Mmbaga
Nipashe
Usafiri mabasi bado shida Ubungo

MAMIA ya abiria bado wamekwama katika stendi kuu ya mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam kutokana na uhaba wa mabasi yanayowasafirisha abiria kwenda mikoani.

Akizungumza na Nipashe jana kwenye stendi hiyo, Meneja wa stendi hiyo, Mkama Chirosa, alikiri kuendelea kuwapo kwa tatizo hilo kipindi hiki cha mwishoni mwa mwaka.

Alisema wanashirikiana na Chama cha Wamiiliki wa Mabasi (Taboa) katika kuhakikisha wanalitatua.

"Napenda kuwashauri wamiliki wa mabasi kuongeza magari kwa kipindi hiki cha sikukuu, pia wakumbuke kuyafanyia ukarabati kabla hawajaanza safari ili kuepusha usumbufu kwa abiria," alishauri.

Alisema kwa kipindi hiki, wameongeza mabasi kutoka 350 hadi 400 yanayotumia stendi hiyo, lakini bado abiria wanakosa usafiri, hivyo wanashirikiana na mamlaka zingine za nchi kuongeza magari kwa kuruhusu mabasi madogo kubeba abiria.

"Tunaipongeza serikali kwa kuongeza usafiri wa treni kwa baadhi ya mikoa ya kaskazini, kwa kiasi fulani imesaidia kupunguza msongamano wa abiria kituoni hapa," alisema.

Linda Haule, mmoja wa abiria waliokwama katika stendi hiyo jana, alisema aliwasili alifajiri lakini hadi inafika saa saba mchana, hakufanikiwa kupata basi la kumpeleka Moshi, Kilimanjaro.

"Magari mengi hayafiki kituoni kwa wakati hali inayopelekea kuwapo kwa msongamano mkubwa wa abiria, jua, vumbi vyote vinatuishia, hapa hakuna sehemu maalum ya kujihifadhi wakati tukisubiria usafiri," alisema.

Habari Kubwa