Jitihada zaidi muhimu kutokomeza malaria

24Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Jitihada zaidi muhimu kutokomeza malaria

UGONJWA wa malaria bado ni tishio kwa watu wengi nchini. Ni ugonjwa ambao umekuwa ukipoteza uhai wa watu wengi mijini na vijijini.

Ni ugonjwa ambao kiwango chake cha  maambukizi kimekuwa kikiripotiwa kupanda na kushuka, hivyo wakati mwingine pale inapoelezwa maambukizi kupungua kuwafanya wengi kupuuza kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Kuchukua tahadhari kimsingi ndio njia muhimu na ya pekee katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo, ambao unatajwa kuwa  umeshaua watu wengi kuliko magonjwa mengine.

Jambo la kutia faraja ni kwamba ripoti ya karibuni imebainisha kwamba maambukizi ya malaria yamepungua nchini. Kwamba kiwango cha maambukizi nchini kimepungua zaidi ya asilimia 50 ndani ya miaka miwili kutoka asilimia 14 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 kwa mwaka 2017.

Ripoti hiyo mpya ilitolewa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi, wakati wa kikao kazi cha kanda kilichojumuisha, waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wafamasia na waratibu wa malaria kutoka kanda tano za mikoa ya Dodoma, Singida, Njombe, Iringa na Morogoro.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutathmini utekelezaji wa shughuli za malaria kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP).

Alisema Tanzania imedhamiria kuutokomeza ugonjwa huo, na kwamba mafanikio yameanza kuonekana kwa kipindi cha miaka kumi sasa kwani mwaka 2010 kiwango cha malaria kilikuwa asilimia 18, lakini sasa ni asilimia 7.3.

Mkurugenzi huyo alisema vifo vitokananvyo na malaria navyo vimepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kwa zaidi ya miaka kumi, na vile vile watu wanaougua malaria na maambukizi mapya nao wamepungua kwa zaidi ya asilimia 67.

Hata hivyo, alisema Tanzania bado inatajwa kama nchi yenye kiwango kikubwa chenye malaria katika nchi za Afrika mojawapo kati ya nchi kumi, ingawa bado ipo fursa ya kuitokomeza malaria nchini.

Pamoja na taarifa hizo nzuri na zinazoleta faraja na matumaini, Watanzania tusibweteke kwamba maambukizi ya malaria yamepungua, bali jambo la msingi ni kuifanya ajenda ya kuutokomeza ugonjwa huo kuwa ya kudumu.

Kimsingi, inawezekana kabisa kuutokomeza ugonjwa wa malaria kwa sababu hatua za kuchukua ni za kawaida kama kulalia vyandarua, kuharibu mazalia ya mbu na kuweka mazingira ya makazi katika hali ya usafi.

Pia elimu endelevu kuhusiana na malaria iendelee kutolewa na serikali pamoja na wadau ili kujenga uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa wa malaria, maambukizi, hatua za kuepukana nayo pamoja na matibabu.

Tunaamini kuwa ushirikiano wa wadau wote na jitihada za kila mmoja zitasaidia kupunguza kiwango cha maambukizi kama si kuutokomeza kabisa ugonjwa huo hatari.

Tunaipongeza serikali na wadau wengine kwa jitihada zao zilizowezesha kupungua kwa kiwango kwa zaidi ya asilimia 50 ndani ya miaka miwili kutoka asilimia 14 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 kwa mwaka 2017.

Hizi ni dalili kwamba hatua zaidi zikichukuliwa na kila mmoja kutimiza wajibu wake, bila shaka ukubwa wa tatizo unajulikana, hivyo Watanzania wengi wajikinge ili kuishi bila kuteswa na malaria.

Habari Kubwa