Kwa hili Chadema ni sawa, swali mlikuwa wapi lakini?

25Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kwa hili Chadema ni sawa, swali mlikuwa wapi lakini?

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilihitimisha uchaguzi wa viongozi wake ngazi ya taifa wiki iliyopita, huku kukiwa na hotuba mbalimbali kutoka kwa wanachama na wageni waalikwa.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.PICHA: MTANDAO

Moja ya hotuba hizo ni ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, ambayo aliitoa mbele wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi, baada ya kutetea nafasi hiyo, atakayoishikilia kwa miaka mingine mitano ijayo.

Kwenye sehemu ya hotuba yake alioitoa katika mkutano huo, Mbowe anasema, wao kama Chadema wameamua chama kisiendelee kuwa cha viongozi bali sasa kiwe ni cha wanachama.

"Chadema chama ambacho tuliamua kwa makusudi kabisa, kwamba chama kisiendelee kuwa chama cha viongozi, chama kiwe cha wanachama," anasema kwenye sehemu ya hotuba yake.

Uamuzi huo ni mzuri, hasa kwa kuzingatia kwamba uhai wa chama ni wanachama tena imara, lakini kikiwa cha viongozi hakiwezi kuwa imara, kitabaki kuwa cha mashabiki tu.

Kama Chadema ndio wameshtuka sasa na kuamua kushusha chama kwa wanachama, basi hii ni sawa na kukumbuka shuka kukiwa kumekucha, kwani kilitakuwa kuwa cha wanachama tangu kilipoanzishwa.

Mtindo wa kufanya chama kuwa cha viongozi ni kosa la kiufundi, ambalo inawezekana kusababisha chama kujulikana juu tu wakati ngazi ya chini hakipo, hivyo kuliona hilo ni hatua nzuri ingawa imechukua muda mrefu.

MANUFAA

Njia kuu ya chama kuwa cha wanachama, ni kujiimarisha kimtandao kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, hatua ambayo inaweza kukifanya kiendelee kuwa imara na kuongeza idadi ya wanachama wapya na kuwa kimbilio la wananchi.

Katika mfumo huu, chama kinaweza kuaminiwa na Watanzania wengi na kukipa kura za kukiwezesha kuunda serikali, kutokana na imani ya wananchi juu ya chama hicho.

Iwapo Mbowe alikuwa na maana ya kwamba kwa muda mrefu Chadema kilikuwa chama cha viongozi, basi uamuzi mpya unaweza kusaidia kukiletea mabadiliko makubwa hapo baadaye.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuongeza wanachama wengi zaidi, kwa vile chama kitakuwa kwa wanachama, ambao kimsingi hawako juu bali wanapatikana ngazi za chini kuanzia kwenye mashina.

Pamoja na kwamba CCM ndiye mpinzani mkubwa wa Chadema, nadhani siyo vibaya kujifunza uzoefu kutoka kwa CCM ambayo imejiimarisha kuanzia ngazi ya chini kabisa ikiwa na wajumbe wa nyumba kumi.

Kujiimarisha kwa CCM kumeisaidia ijulikane hadi kwa watoto wadogo, hivyo si vibaya kuiga uzoefu huo na kuufanyia kazi kwa kutambua kuwa kwa kawaida wanachama wako ngazi ya chini.

Mfumo huo umekifanya Chama tawala kuendelea kushika dola licha ya upinzani mkali kutoka vyama vingine vya siasa, kwani kimejiimarisha kuanzia ngazi ya chini.

Inawezekana ndiyo maana ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika kikitanguliwa na African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, hivyo si vibaya vyama vingine kuiga mfano na ikiwezekana ukaboreshwa pale inapoonekana kuna kasoro.

Kwa kuwa chama hicho kimemaliza uchaguzi na kusema kimeamua kwa makusudi kiwe ni cha wanachama, basi hilo liandane na ubunifu wa kukiwezesha kuwa imara zaidi.

CHANGAMOTO

Chama kutokuwa cha wanachama kuna matatizo yake ikiwamo viongozi kutowajibika kwa wanachama na kutotii kile ambacho wanachama wanataka, bali kuamua mambo wanavyotaka wenyewe.

Lakini chama kikifuata mfumo wa kuwa cha wanachama, utasaidia kujiimarisha, kutokana na ukweli kwamba kisiasa mfumo huo unafanana na maendeleo ya nchi ambayo yanategemea kodi za wananchi.

Hivyo maendeleo ya chama yanategemea ada za wanachama na michango mingine, ambayo ni muhimu, na kama viongozi wa Chadema wamegundua kosa na kuchukua hatua hizo, ni sahihi ingawa wamechelewa.

Bila kuchukua hatua hizo, matokeo yake ni chama kutotii sauti au matakwa ya wanachama, ambao kimsingi ndiyo wenye chama na kubaki kusikiliza tu kile ambacho viongozi wanaamua bila wao kushirikishwa.

Ni muhimu chama kujitegemea kwa fedha na katika mambo mengi, kwa kutumia wanachama wake kama, ambavyo ni wajibu kwa chama cha siasa kuwatumikia wanachama wake na wananchi kwa ujumla.

Hayo yote kama nilivyosema, hayana budi kuendeshwa kwa kutegemea zaidi michango ya wanachama, si kuwa na mashabiki tu, ambao wakati mwingine wanaweza kukimbia kwa vile hawana uchungu na chama.

Lakini ni lazima uendeshaji wa chama cha siasa ulingane na hali ya kiuchumi ya chama chenyewe na wanachama kwa ujumla na si kuwakamua kutoa hata kile wasichokuwa nacho.

HISTORIA

Historia inaonyesha kuwa Chadema ilianzishwa mwaka 1992, ikiwa chini ya uenyekiti wa aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei, ikiwa na falsafa ya nguvu ya umma.

Kwa imani kwamba umma ni sehemu ya serikali inayotoa ridhaa ya maamuzi na ruhusa ya mfumo wowote huku itikadi ikiwa ni mlengo wa kati unaoamini katika soko huria lenye kusimamiwa.

Baadaye mwaka 1998 nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho taifa ilichukuliwa na Bob Makani ambaye alishika wadhifa huo hadi mwaka 2003 alipomaliza muda na kuamua kuendelea na kazi zake kama mwanasheria wa kujitegemea.

Mkongwe huyo alibaki kuwa kiongozi na mshauri wa chama hadi alipokutwa na umauti huku nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa ikiwa tayari imeshachukuliwa na Mbowe, ambaye hadi sasa ni mwenyekiti.

Chama kilianza kushiriki uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995, na katika uchaguzi huo kilipata wabunge wanne na madiwani 42.

Uchaguzi wa mwaka 2000, chama hicho kilipata wabunge watano na madiwani 75, kisha uchaguzi wa mwaka 2005, chama hicho kiliendelea kuongeza idadi ya wabunge wakafikia 19, huku madiwani wakiwa ni 103 na uchaguzi wa mwaka 2010 kilipata wabunge 24, na mwaka 2015 kikavuna wabunge 34.

Habari Kubwa