Siku zilizobaki zitumike ipasavyo usajili wa simu

25Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Siku zilizobaki zitumike ipasavyo usajili wa simu

Hatimaye muda uliotolewa na serikali kwa wamiliki wa laini za siku kuzisajili kwa mfumo wa alama za vidole umefikia ukingoni.

Ni ukingoni kwa sababu zimebaki siku saba kuanzia leo hadi siku ya mwisho ambayo ni Desemba 31.

Sharti la kusajili laini ya simu ni kwamba mmiliki anatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa. Kwa ligha nyingine ni kwamba hakuna mmiliki wa kaini ya simu anayeweza kuisajili bila kuwa na kitambulisho cha taifa.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana serikali imekuwa ikiwahimiza wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho vya taifa kutokana na umuhimu wake, ikiwamo kuvitumia kusajili laini za simu.

Hata hivyo, licha ya kuripotiwa taarifa mbalimbali kwamba kwenye maeneo kadhaa nchini wananchi wengi hawajapata vitambulisho vya taifa, hivyo kukwama kusajili simu zao, lakini kwa wale ambao wamepata vitambulisho hivyo au namba hawanabudi kuzitumia siku chache zilizobakia kusajili laini zao za simu.

Haiingii akilini kusikia kuwa maelfu ya wananchi hawajasajili laoni zao wakati umebakia muda mfupi.

Inawezekana wapo wanaokwazwa na kutokuwa na vitambulisho au namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), lakini pia wapo wale ambao wana tabia ya kujitokeza siku za mwisho na kusababisha usumbufu mkubwa hususan misongamano katika maeneo ya kusajili laini za simu.

Usajili wa laini za siku kwa mfumo wa alama za vidole ni muhimu kwa sababu bila kusajili laini simu itazimwa na mmiliki atakosa huduma muhimu kama mawasiliano na kufanya miamala.

Ili kuepukana na athari hizo, ni vyema kila mmiliki wa simu kwenda kusajili laini katika ofisi za kampuni za simu na za mawakala ambazo zinaendelea kutoa huduma hiyo.

Wapo wanaodhani kuwa serikali itaongeza muda. Hata hivyo, serikali imeeendelea kusisitiza kuwa muda hautaongezwa, na ikifika Desemba 31 laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa kwa mfumo wa alama za vidole zitazimwa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, juzi alisema kuwa amebakiza siku nane kutekeleza uamuzi huo wa serikali.

Kamwelwe alisema hakuna tatizo linalowazuia watu washindwe kusajili, na kwamba watakaoshindwa kufanya hivyo, watakuwa wamekaidi, hivyo watakakosa mawasiliano.

Alisisitiza kuwa suala hilo si la masihara, na badala yake watazifungia laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Mmlaka ya Mawasiliano TCRA, James Kilaba, alisema watu milioni tatu wana namba za usajili za Nida lakini hawajajitokeza kujisajili.

Alisema kati ya watu hao wenye namba za vitambulisho, wanatarajiwa kusajili laini milioni 5.6 kwa sababu mtu mmoja anamiliki zaidi ya laini moja.

Aidha, laini zilikuwa zimesajiliwa hadi Desemba 10, mwaka huu, zilikuwa 47,063,603, ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1. Idadi ya laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole zilikuwa 19,681,06 sawa na asilimia 42 zinazomiliwa na watu Sh. milioni 7.6.

Ni matarajio yetu kuwa ifikapo Desemba 31 kila mmiliki wa laoni ya simu ambaye ni makini kwa kuelewa athari za kuzimiwa simu atakakikisha anajitokeza kusajili kabla ya muda uliopangwa.

Kwa wananchi ambao wameshindwa kupata vitambulisho na mamba za Nida kwa sababu za msingi, tunaamini kuwa serikali itaangalia njia nzuri za kuwasaidia wapate namba au vitambulisho ili wasajili laini na waendelee kupata huduma za mawasiliano.

Habari Kubwa