Wakulima kufanywa daraja la mapato halmashauri liangaliwe

25Dec 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Wakulima kufanywa daraja la mapato halmashauri liangaliwe

LIKIZO aliyoifanya Muungwana hivi karibuni katika mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Maswa, imezidi kumfumbua macho zaidi juu ya changamoto ambazo bado wakulima na hasa wadogo wanakumbana nazo.

Na hiyo ni pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano zikilenga kuhakikisha kwamba, maslahi ya kundi hilo miongoni mwa Watanzania takribani milioni 55, sasa yanalindwa kwa udi na uvumba.

Ni katika ile dhima ya kuhakikisha jasho lao wanalolitoa kwenye uzalishaji wa shughuli hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi, linawafaidisha kupitia pamoja na mengine, bei nzuri sokoni ya mazao wanayozalisha.

Kwamba haiishii katika suala la bei nzuri sokoni, lakini pia hata kwenye mahitaji yao mengine yanayoboresha kilimo chao, kama huduma za ughani, pembejeo kwa maana ya bei nzuri ya mbegu, mbolea, dawa, huku upatikanaji ukiwa hauna mazonge.

Muungwana anasema kwa changamoto alizozishuhudia, bado Rais John Magufuli na wasaidizi wake wakuu, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wana kazi kubwa ya kufanya katika dhamira yao ya kuona ustawi wa wakulima nchini.

Likizo hiyo imemfumbua macho Muungwana kuona ukweli kwamba kumbe bado wakulima ni mtaji na chanzo kikubwa kwa baadhi ya halmashauri nchini ambazo huvuna fedha isivyo kihalali kutoka kwa mauzo ya mazao yaliyofanywa na wakulima.

Changamoto kubwa ambayo Muungwana ameipigia kelele kwa muda mrefu ilikuwa ni ya wakulima wa pamba na hasa Kanda ya Ziwa kutolipwa fedha zao toka walipouza pamba yao msimu uliomalizika karibuni.

Kwamba kuna wakulima ambao walikuwa hawajalipwa fedha kwa zaidi ya miezi minne toka walipouza pamba, kisha ikachukuliwa na kampuni za ununuzi wa zao hilo maeneo mbalimbali nchini.

Ni vyema kwamba ahadi ya serikali kuwa wakulima wote wanaodai fedha zao watalipwa ifikapo Desemba hii imetekelezwa kwa sehemu kubwa na Muungwana ni shuhuda wa hili katika kijiji alikokuwa likizo.

Lakini si katika kijiji hicho, lakini hata kwenye vijiji vya jirani, wilaya na mkoa karibu wote wa Simiyu bila kusahau mikoa jirani ya Shinyanga, Mwanza na Geita, ambako nako ana taarifa za uhakika kwamba wakulima wamelipwa fedha zao.

Pamoja na serikali kusimamia hilo na kampuni za ununuzi kulipa wakulima, bado utaratibu uliowekwa na baadhi ya halmashauri kwa madai ya kukusanya fedha za pembejeo walizochukua wakulima si muafaka kwa maoni ya Muungwana.

Kwa mfano Halmashauri ya Maswa ilielekeza kampuni za ununuzi kupeleka fedha walizokuwa wanadai wakulima wa pamba katika halmashauri hiyo, badala ya kuzipeleka moja kwa moja kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS).

Sasa halmashauri ndiyo iliyokuwa inatoa maofisa wa kwenda kulipa wakulima ili waweze kukusanya fedha za pembejeo walizowakopesha wakulima msimu uliopita wa kilimo.

Muungwana hana shida na utaratibu huo, ingawaje ulikuwa unachelewesha fedha za wakulima bila sababu, shida yake ni kwamba makato ya

pembejeo yaliyokuwa yakifanywa yalikuwa ni ya kukadiria, kwani hakukuwa na nyaraka zinazoonyesha mkulima husika alichukua nini na kwa kiwango gani.

Hivyo kilichokuwa kikifanyika ni kwa maofisa hao kuangalia mkulima amepata shilingi ngapi na kisha kuamua akatwe kiasi fulani kutoka kwenye fedha zake na ilipotokea mkulima kupinga makato hayo, aliambiwa aache fedha zake, walipwe wengine.

Kwa 'usawa' huu ambapo mkulima alishakaa miezi akisubiri fedha hizo, hakuna mkulima kimsingi aliyekuwa tayari kuendelea kukataa makato hayo, zaidi ya kuyakubali kama yalivyokuwa yanabainishwa na maofisa wa halmashauri.

Matokeo yake wakulima wamekatwa fedha nyingi zaidi ya kile ilivyostahili kulipia mikopo ya pembejeo, hivyo halmashauri kufaidika kupitia mgongo wao.

Ni maoni ya Muungwana kwa serikali kwamba itupie jicho changamoto hii, ili

wakulima wasiendelee kuwa daraja la halmashauri na watendaji wengine serikalini la kuvuna fedha isivyo kihalali kutoka kwao.

Habari Kubwa