Aonya wanaoshabikia utoaji mimba, 'unga'

26Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Aonya wanaoshabikia utoaji mimba, 'unga'

UTOAJI wa mimba, matumizi ya njia za kudhibiti mimba, dawa za kulevya na mafarakano katika ndoa, yametajwa kuwa baadhi ya matendo ambayo watu wanayashabikia bila kujua kuwa wanatenda dhambi.

Kauli hiyo ilitolewa na Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu Nundu, Jimbo Kuu la Mwanza, Padri Moses Mapela, wakati wa misa ya mkesha wa Krismasi.

Alisema vijana wa sasa pia wanatumia vilevi vinavyowafanya washindwe kufanya kazi huku wengine wakiona kutoa mimba ni jambo la kawaida.

"Leo watu tunashabikia utoaji wa mimba, tunaua watoto wachanga wasio na hatia, tena kwa kukusudia, tunatumia dawa za kudhibiti mimba mradi tuwe huru na bado tunafika hatua tunasema ni haki ya msingi ya mwanamke, haya ni matendo ya giza," alikemea.

Padri Mapela alisema katika zama hizi, watu wanadhulumiana, wanauana, wanatesana na kuoneana vijicho, katika familia amani hakuna, ugomvi kila wakati, na muda mwingine wazazi wanagombona mbele ya watoto.

Alisema katika zama hizi, wazazi pia hawawafundishi watoto wao maadili mema na kuongeza kuwa matendo hayo ndiyo yanarudisha watu kwenye giza totoro.

"Wanandoa wakati mwingine tunaishi familia moja, hatuongeleshani, hatusemeshani, na wakati mwingine baba au mama anapofika nyumbani, anajisikia na kujiona kana kwamba sasa amejikabidhi tena katika Gereza la Butimba au Segerea ama la Keko, kwa sababu ndani hakuna upendo, furaha, maelewano. Sasa hii utaiita ni familia, au ndoa ama ndoana?" Alihoji.

Alisema katika familia zinapaswa kuishi kwa amani, furaha na kufurahia uwapo wa mwanafamilia, huku baba na mama wanapowaona watoto wawapende, wawathamini na kuwajali na kuwapa mafundisho yatakayowatoa gizani na kuwapeleka kwenye mwanga.

"Kuzaliwa kwa mwokozi, kuzaliwa kwa masihi, kutufundishe sasa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano kama ambavyo tunavyoiona familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu," alisema.

Habari Kubwa