Staili hii enyi Machinga ni hatari kwa usalama wenu

26Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Staili hii enyi Machinga ni hatari kwa usalama wenu

BAADHI ya wafanyabiashara wadogo wa Kimara Mwisho, Dar es Salaam wako katika hatari kutokana na kufanya shughuli zao, chini ya nyaya kubwa za umeme wakati wa usiku.

Muda mrefu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilishaweka tangazo la kupiga marufuku wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao eneo hilo, kwa vile ni hatari kwa usalama wao.

Kuanzia asubuhi hadi jioni huwa hawaonekani kwenye eneo hilo, lakini inapofika usiku ndio wanamiminika kwa wingi wakiendelea na biashara kama kawaida, kana kwamba muda huo hakuna hatari inayoweza kuwapata.

Hatua zilizochukuliwa na Tanesco, inalenga kuwaondoa mahali hapo na kuwaacha wafanye salama, kwani ukweli unabaki palepale, kwamba eneo hilo ni hatarishi. Mtindo wa kuvizia hadi usiku ni sawa na kudanganya usalama binafsi.

Ndugu zangu hawa, pamoja na kutambua ukweli wanatafuta maisha, bado wangepaswa kuzingatia usalama wao kwanza. Ukweli usiopingika, uhai ni zaidi ya biashara zao, kwani walioamua kuwaondoa kwenye eneo hilo wanajua madhara yake na vyema wakazingatia maoni yao kwa ajili ya usalama wao, sasa na baadaye.

Yapo mengine ya kupuuzia kuliko hilo, ambalo linagusa uhai wao na hivyo suala la visingizio kwamba ‘wakafanye biashara wapi’ lisiwe na nafasi vichwani mwao, kwani mchana huwa wako wapi?

Ninasema hivyo, kwa sababu imekuwa kawaida kwa baadhi ya wajasiriamali na wachuuzi wadogo, wanaojenga tabia ya kuhoji swali kama hilo, mara wanapotakiwa kuhama kwenye maeneo ambayo siyo rasmi kwa shughuli zao.

Wapo waliokwishawahi kuhoji kwamba ‘wakafanyie biashara zao wapi’ baada ya kuondolewa chini ya nyaya za umeme eneo la Ubungo, bila ya kuhoji upande wa pili kuhusu hatari iliyowakabili.

Hatari inayowanyemelea ni kubwa zaidi, ingawa zipo nyingine kama za kufanya biashara kando ya barabara na kutupa taka ovyo kwenye maeneo mbalimbali na kuchafua mazingira.

Umefika wakati, wafanyabiashara wenyewe wajiongeze na kuchukua hatua haraka kabla ya kukumbwa na madhara na kuanza kulalamika kwamba ‘serikali imewaacha’ na kumbe tatizo liko kwao wenyewe.

Watambue kwamba, eneo hilo chini uya nyaya ni hatari zaidi kwa usalama wao wakati wote, siyo kwamba halifai mchana na kisha usiku linafaa, hapa wenye mawazo hayo watakuwa wanajidanyanga.

Ni vyema wakaogopa hatari inayoweza kuwapata kuliko kuiogopa Tanesco, ilikwishaamuru watoke katika eneo hilo, kwa ajili ya usalama wao na wakawekewa bango linaloonyesha hatari inayoweza kuwapata.

Kitendo cha wao kufanya biashara usiku, kinaonyesha kwamba wanahofu hatua za watumishi wa Tanesco kuwakuta na inapotimia usiku, wanajua kuwa siyo muda wa kazi hivyo watumishi hao hawawezi kufika eneo hilo.

Hapa jambo la msingi ni kuepuka hatari inayoweza kusababishwa na nyaya hizo, siyo watumishi wa Tanesco, hivyo wamachinga watafakari na kuchukua hatua haraka za kutorudi kwenye eneo hilo hatarishi.

Vilevile, wenye jukumu la kuboresha masoko ya wafanyabiashara wadogo, waharakishe kufanya kazi hiyo, ili kusaidia kuepusha hatari inayonyemelea wale wanafanyia biashara kwenye maeneo ya hatari.

Ucheleweshaji wa kuboresha masoko hayo, pia unaweza kuchangia kuinyima serikali mapato yanayotokana kodi au ushuru kutoka kwa wafanyabiashara, ambao wamekuwa wakilalamikia ubovu wa masoko yao.

Kimsingi, kuna hatari zinazoweza kusababishwa na mambo matatu niliyoyataja awali. Hivyo, suala la kuwapo masoko rasmi ya wamachinga ni jambo la msingi.

Pia usafi wa mazingira kwenye maeneo yanakofanyiwa biashara, ikizingatiwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanadiriki kujisaidia haja ndogo katika chupa za plastiki na kuzitupa ovyo mitaroni.

Wengine wanapanga biashara zao kwenye mitaro au kuchimba kingo za barabara na kuweka vibanda kwa ajili ya kuweka bidhaa wanazouza.|

Ni mtindo unaochukua nafasi kwa biashara za kando ya barabara, ambayo nayo siyo salama, kwani ni jirani na mazingira ya ajali. Gari linaweza kupata tatizo na kumshinda dereva, matokeo yake ni kuwavaa wafanyabiashara walioko hapo.

Hivyo, ni vyema ndugu hao wajitahidi kufanya shughuli zao kwenye mazingira salama, badala ya kulzimisha hata pale pasipofaa na mwisho wa siku wanaangukia kwenye matatizo na kulalamika kwamba hawasaidiwi.

Habari Kubwa