Abiria wakoshwa treni Dar-Moshi

27Dec 2019
Maulid Mmbaga
Nipashe
Abiria wakoshwa treni Dar-Moshi

ABIRIA wanaosafiri kwa treni ya Dar es Salaam-Moshi, wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo iliyorejeshwa mwanzoni mwa mwezi huu, baada ya kusimama kwa miaka 25.

Treni hiyo ilianza tena safari zake Desemba 6, mwaka huu, safari moja kwa sasa ikichukua zaidi ya abiria 600 na imepunguza adha kwa wananchi hasa wazaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro ambalo wana utamaduni wa kurejea walikozaliwa kwa ajili ya mapumziko ya mwishoni mwa mwaka.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema jana kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha inaboresha huduma ya usafiri huo hususani kipindi hiki cha sikukuu.

Alisema katika mikakati yake, serikali imeagiza mabehewa 44 ili kukidhi mahitaji kwa kuwa kumekuwa na idadi kubwa ya abiria kwa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

"Ruti ya kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi ni Jumanne na Ijumaa, Moshi kwenda Dar ni Jumatano na Jumamosi, safari inaanza saa 10:00 alasiri na kufika 2:00 asubuhi," alisema.

"Ruti ya Moshi tulitakiwa tupeleke treni kila siku. Jana (juzi) tulibeba abiria 950, kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi, hivyo ni dhahiri kwamba uhitaji wa huduma hii ni mkubwa," alibainisha.

Alisema huduma ya usafiri wa treni itaendelea kutolewa pia katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Kigoma ikiwa ni jitihada za serikali katika kurahisisha usafiri kwa wananchi.

Mmoja wa abiria wa treni ya Dar es Salaam kwenda Moshi, Eveline Lyimo, aliipongeza serikali kwa kurejesha usafiri huo kwa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kusitishwa kwa miongo miwili na nusu.

Alisema huduma hiyo imesaidia kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi, ikizingatiwa ni utamaduni wa wazaliwa wa Kilimanjaro kurejea nyumbani mwishoni mwa mwaka.

Alisema huduma inayotolewa katika usafiri huo ni nzuri na nauli zake ni himilivu, akisifu uongozi kwa kuweka kiwango kinachoendana na hali halisi ya maisha ya Watanzania walio wengi.

"Nauli ni Sh. 10,700 kwa daraja la tatu, Sh. 15,300 daraja la pili la kukaa na 25,400 la pili la kulala," Lyimo alibainisha.

Aliongeza kuwa miaka ya nyuma, kipindi kama hiki, kiwango cha nauli ya mabasi kilikuwa kinapanda kutoka Sh. 25,000 hadi 38,000 kwa kila abiria, hivyo treni imeokoa fedha zao.

Isack Gaspar, mhudumu katika treni hiyo, aliwashukuru Watanzania kwa kuwaamini na kutumia usafiri huo.

"Ndani ya treni tunatoa huduma ya nyama choma na vinywaji na tulikuwa tunabeba kreti 50 za vinywaji ila kwa sasa tunachukua zaidi ya 150, kutokana na idadi ya abiria kuwa kubwa," alisema.

Habari Kubwa