Simba yapanga hesabu Ligi Kuu

27Dec 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Simba yapanga hesabu Ligi Kuu

ZIKIWA zimebakia siku chake kabla ya watani wa jadi kukutana kwa mara ya kwanza katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema kuwa bado kikosi chake hakijaanza kuufikiria mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa ifikapo Januari 4, mwakani.

Simba, inatarajia kushuka dimbani kesho kuwavaa KMC FC na Desemba 31, mwaka huu, itafunga mwaka kwa kuwakaribisha Ndanda FC, kutoka mkoani Mtwara.

Akizungumza na gazeti hili, Matola, alisema kuwa nguvu na akili zao kwa sasa ziko katika kuhakikisha wanashinda mechi mbili zilizo mbele yao na baada ya hapo, ndio wataanza mipango ya kuwakabili Yanga.

Matola alisema kuwa mechi zote za Ligi Kuu ni muhimu na ili timu iweze kutwaa ubingwa, inatakiwa kukusanya pointi nyingi.

"Kwanza kabisa tunamshukuru Mungu kwa kumaliza mechi salama, haikuwa mechi nyepesi, tumelazimika kubadilisha mbinu ili kupata ushindi, kuhusu Yanga, siwezi kuizungumzia kwa leo (juzi), tuna mechi nyingine hapo katikati, lakini kila mechi huwa na mipango yake," alisema Matola.

Nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo aliongeza kuwa kila siku kikosi hicho kinaendelea kuimarika na wanaamini malengo yaliyowekwa na vinara hao wa Ligi Kuu Bara yatatimia.

Habari Kubwa