Ni wakati mwafaka kuachana kabisa na uagizaji mbegu nje

27Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Ni wakati mwafaka kuachana kabisa na uagizaji mbegu nje

UPATIKANAJI wa mbegu bora za kilimo umekuwa moja ya changamoto ambazo zinawakwaza wakulima wetu.

Wakulima wengi wakati mwingine wanashindwa mahali za uhakika pa kuzipata, lakini gharama yake ni kubwa, hivyo kuwa miongoni mwa sababu za kushindwa kuzipata. 

Hata hivyo pamoja na changamoto ya upatikanaji wa mbegu za kisasa kwa wakulima wetu nchini, katika miaka ya karibuni zimekuwapo jitihada mbalimbali ambazo zinaendelea za uzalishaji wa mbegu za kisasa zinazofanywa na taasisi zetu za utafiti wa kilimo.

Taasisi hizi zinaendelea kuzalisha mbegu bora na za kisasa za mazao mbalimbali ya chakula na biashara, hivyo kuashirika kwamba nchi yetu kwa sasa haina sababu za kuagiza mbegu kutoka nje.

Pengine ni kutokana na jitihada hizi, serikali imeona kuwa kwa sasa hakuna sababu za kuendelea kuagiza mbegu kutoka nje kwa kutumia fedha nyingi.

Kutokana na hali hiyo, serikali ilieleza mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa imekusudia kuanzisha juhudi wezeshi kuwezesha mbegu bora za kilimo kuzalishwa nchini ili kuondokana na wimbi la uagizaji wa mbegu nje ya nchi.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, baada ya kutembelea kampuni ya Namburi inayojihusisha na uzalishaji wa mbegu za mahindi, mtama na mpunga iliyopo katika eneo la Vwawa wilayani Mbozi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe.

Alisema kuwa Tanzania ina uhitaji wa mbegu kiasi cha tani 186,000 za mazao mbalimbali, huku uzalishaji wa ndani ikiwa ni pamoja na uagizaji wa mbegu nje ya nchi ukiwa bado mdogo kwani haujafika hata tani 50,000.

Alibainisha kuwa Tanzania ina maeneo makubwa na bora kwa uzalishaji, hivyo ni lazima kuzalisha mbegu za kutosha nchini na kuachana na utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.

Waziri Hasunga aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa wananunua mbegu bora kwa ajili ya kukabiliana na msimu wa kilimo na kuachana na matumizi ya mazao yao ya misimu iliyopita waliyoyahifadhi kama mbegu.

Kutokana na jitihada na kasi kubwa ya utafiti na uzalishaji wa mbegu bora nchini, tunaona kwamba uamuzi wa serikali wa kuagiza mbegu kutoka nje ni hatua nzuri ya kuboresha kilimo chetu nchini.

Kilimo hiki ndicho tegemeo la kusapoti viwanda ambavyo vimeanza kujengwa kwa lengo la kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kwa hiyo kama taifa ni hatua nzuri ya kuachana na utaratibu wa kuagiza mbegu kutoka nje ambao hauna tija kwa sababu miongoni mwa kasoro zake ni kuagiza kiasi ambacho hakilingani na mahitaji halisi.

Kibaya zaidi ni kuwa uhaba wa mbegu bora na za kisasa unawafanya wakulima kutegemea mbegu walizozizalisha misimu ya nyuma, ambazo mara nyingi hazina ubora na matokeo yake ni kuchangia kushuka kwa mavuno kila mwaka.

Tunaamini kuwa serikali haitarudi nyuma katika uamuzi wake wa kujielekeza katika uzalishaji wa mbegu baada ya kuziagiza nje.

Ushauri wetu ni kuwa serikali katika kutekeleza mpango huu ishirikishwe taasisi za utafiti wa kilimo ambazo zimefanya utafiti wa kina wa mbegu pamoja na kuzizalisha. Kwa kufanya hivyo tutazalisha mbegu bora na za kukidhi mahitaji ya wakulima nchini.

Aidha, utekelezaji wa mpango huu uwashirikishe maofisa ugani wetu kwa kiwango kikubwa, ikiwamo kuwapeleke kwa wakulima kwa ajili ya kuwapa elimu kuhusu matumizi ya mbegu hizo.

Habari Kubwa