Kampeni hizi zinaweza 'kufuta' jembe la mkono

27Dec 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Kampeni hizi zinaweza 'kufuta' jembe la mkono

KILIMO cha kutumia jembe la mkono na kinachotegemea mvua za msimu ndicho kinachotumiwa na wakulima nchini na kwa namna moja au nyingine, kinachangia kukwamisha maendeleo yao.

Kutokana na hali hiyo, wadau wa kilimo kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakiendesha mikakati ya kuwezesha kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji.

Serikali nayo iko katika mkakati wa kuondoa jembe la mkono, ili wakulima watumie matrekta yanayoweza kuwafanya wakidhi mahitaji kwenye kilimo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Profesa Damian Gabagambi, alikaririwa na vyombo vya habari kwamba NDC, inataka jembe la mkono libaki katika Makumbusho ya Taifa.

Hatua hizo za NDC ni nzuri, kwani zina mwelekeo wa kusaidia kumkomboa mkulima kutoka katika matatizo anayokabiliana nayo kwa jembe la mkono na kutegemea mvua za msimu.

Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inasema zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania ni wakulima wengi wa wanatumia jembe la mkono na kutegemea mvua za msimu kwa ajili ya kilimo.

Kilimo cha kutegemea jembe la mkono hakiwezi kukidhi mahitaji ya chakula au kwenye mazao ya biashara, hivyo ni muhimu wakulima waachane na jembe hilo ambalo limekuwapo tangu nchi ipate uhuru.

Suala la uimarishaji wa kilimo linasisitizwa sana na serikali, kwani hata Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewahi kusema, ni moja kati ya juhudi za serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi katika taifa.

Asilimia 75 ya wananchi wanajihusisha na kilimo, mifugo na uvuvi nchini na kusisitiza, serikali itaendelea kuzipa kipaumbele sekta hizo na kuongeza bajeti, ili ziongeze pato la taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Serikali imeweka mikakati inayolenga kusaidia uimarishaji wa shughuli za kilimo kwa kuongeza matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491 mwaka 2005/2006 hadi 16,478 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, hivyo kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 12.

Nikirejea kwenye lengo langu ni kwamba, wakati serikali ikiwa na mpango wa kuongeza matrekta, mmoja wa wadau wa kilimo Prof. Sospeter Muhongo amekuja na mkakati wa kuwatua wakulima jembe la mkono jimboni mwake.

Mkakati huo ni kugawa majembe 20 ya kukokotwa na ng'ombe (plau), kwenye vijiji vya Jimbo la Musoma Vijijini, lengo ni kuhakikisha wakulima wanaachana na jembe la mkono.

Mbunge huyo aligawa katika vijijini 20, kati ya 68 vinavyounda jimbo hilo, huku akijipanga kuendelea zaidi hapo baadaye ili kuhakikisha wakulima wote jimboni wanatumia jembe la kukokotwa na ng'ombe.

"Tumeanza rasmi kampeni za kuachana na jembe la mkono ikiwa ni mwelekeo wa kwenda kwenye trekta, lakini tunaanzia plau kwanza, ambazo nimegawa katika vijiji 20," anasema Profesa Muhongo.

Alipotoa msaada wa plau, kuna utaratibu wa kukopa matrekta unaoendelea ambao unaandaliwa na Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Musoma, kwa ajili ya vyama vya ushirika vya msingi vilivyopo.

"Musoma Vijijini lina jumla ya vyama 35 vya ushirika vya msingi vya ushirika na halmashauri iko tayari kuvisaidia kutayarisha nyaraka za kutafuta mikopo ya kununulia matrekta kwa manufaa ya wanachama," anasema.

Inajulikana, plau zina uwezo wa kulima eneo kubwa kwa muda mfupi kuliko jembe la mkono, hivyo hatua ya wakulima kugawiwa majembe hayo, itasaidia kuwarahisishia shughuli za kilimo.

Majura Mbogora, ni mkulima wa kijiji cha Bukumi, anayesema, kwa kutumia plau, anaweza kulima ekari moja kwa siku moja badala ya siku tano hadi saba, ambazo anatumia jembe la mkono.

Anasema, kupatikana kwa majembe ya kukokotwa na ng'ombe ni mojawapo ya hatua muhimu kwa ajili ya kupanua ukubwa wa mashamba yao ambayo watayalima kwa kutumia muda mfupi.

Habari Kubwa