Usajili wachezaji dirisha dogo usifanyike kishabiki

28Dec 2019
Mhariri
Nipashe
Usajili wachezaji dirisha dogo usifanyike kishabiki

WAKATI mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kukamilika hivi karibuni, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeshafungua dirisha dogo la usajili wa wachezaji wapya wanaotarajiwa kuongezwa katika ligi hiyo.

Ligi hiyo ndiyo ya juu kwa upande wa Tanzania Bara, na ndiyo inayotoa mwakilishi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo hufanyika kila mwaka chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Licha ya dirisha hili na kipindi hiki cha usajili kuonekana kuwa kidogo, lakini ni muhimu kwa makocha kuongeza umakini kwa sababu ya kuimarisha vikosi vyao.

Ni usajili ambao unatakiwa kufanywa kwa kuzingatia mahitaji halisi na muhimu kwa timu husika ili iweze kutimiza malengo yake.

Wakati baadhi ya timu zikiwa na mechi za viporo mkononi, lakini ni wazi kwamba klabu karibu zote tayari zimeshabaini mapungufu yaliyoko kwenye vikosi vyao, na huu ndio wakati sahihi wa kutibu matatizo hayo, ili kurejea kwenye ushindani wakati wa mzunguko wa pili au lala salama.

Nipashe inawakumbusha viongozi wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu ya Wanawake, kuwaacha makocha wafanye kazi zao kwa weledi, ili mwisho wa msimu, timu hizo ziweze kupata matokeo mazuri.

Hiki ndio kipindi ambacho, maoni na mapendekezo ya makocha yanatakiwa kufuatwa kama sio asilimia 100, basi angalau iwe asilimia 60, na hapo, ndipo mwisho wa msimu mnaweza kuzungumza lugha moja kama sio kufungua mvinyo kwa furaha.

Najua ni ngumu kwa baadhi ya timu, kutekeleza mapendekezo ya makocha wao, kutokana na hali halisi ya kiuchumi, lakini hali hii haitoi baraka au haimaanishi viongozi wachukue jukumu la kusajili wachezaji au kuwaacha baadhi ya nyota kwa matakwa yao binafsi.

Tunawakumbusha kuwa, kama klabu zetu zinataka kweli kushindana na kufanya vema katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho na Kombe la Kagame, usajili wa "mihemuko" au kukomoana hasa kwa vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga, umepitwa na wakati.

Umefika wakati viongozi wa klabu wanatakiwa kuwaamini makocha wao na kutoweka shinikizo la aina yoyote kwenye mchakato huu muhimu, kwa kuamini uzoefu na elimu walizonazo makocha hao, zitafanikisha kufikia malengo ya timu husika.

Endapo timu itashindwa kutumia vema kipindi hiki cha dirisha dogo, hali inaweza kuwa mbaya na ikikumbukwe kwamba, idadi ya timu zitakazoshuka daraja msimu huu zimeongezeka.

Ingawa idadi ya mechi ambazo hazijachezwa ni nyingi, lakini tayari klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimeshajigawa katika makundi mawili, zipo zinazowania ubingwa na zile zinazopambana kujiepusha na janga la kushuka daraja.

Picha hii inatakiwa kutumiwa kigezo cha kila klabu kutumia wakati huu wa dirisha dogo, kufuta makosa yaliyojitokeza na hatimaye kuanza mzunguko wa pili kwa kuwa na vikosi imara ambavyo vitapambana kusaka matokeo chanya.

Ikumbukwe ligi hii ndiyo inayotegemewa kuimarisha na kutoa nyota watakaopeperusha bendera ya Tanzania katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazofanyika Aprili mwakani.

Ni ukweli usiofichika, mafanikio ambayo tunayaona leo katika timu za Ulaya au za hapa Afrika kama TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hayatokani na vitendo vya miujiza, ni matunda ya kufanya kazi kwa weledi, bila kusahau uwezo wa kifedha wa klabu ni sihala namba moja ya kufikia malengo.

Habari Kubwa