Umbea wa viongozi unaharibu

28Dec 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Umbea wa viongozi unaharibu

UMBEA/umbeya ni tabia ya kutoa habari bila kutumwa au kuulizwa; udaku udakuzi; tabia ya kufuatilia au kusikiliza habari za watu wengine bila kutumwa.

‘Uongozi’ ni madaraka anayopewa mtu ya kusimamia au kuongoza shughuli; dhamana ya kusimamia jambo kwenye taasisi au penginepo. Hapa nawazungumzia viongozi wa vilabu vya kandanda, hususan Simba na Yanga.

‘Vizabizabina’ ni watu wanaofitini watu wa pande mbili zinazohasimiana, wenye tabia ya kuchochea uhasama baina ya watu wa pande mbili.

Mambo yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa Simba na Yanga ndio yasababishayo mvutano baina ya timu hizo wakati wa usajili wa wachezaji. Mambo ya siri yanayojadiliwa kwenye mikutano ya ndani, huelezwa kwa baadhi ya wanachama na waandishi wa magazeti kwa masharti ya kutotajwa majina yao.

Kama ni lazima kuwekwa hadharani, kuna wasemaji maalumu walioajiriwa kueleza mambo muhimu ya vilabu kama ni lazima. Hao wanaojitia kimbelembele kutoa siri za vilabu ni wambea na wazandiki (watu wasio wakweli, waongo, wanafiki na wadanganyifu.)

Wahenga waliuliza: “Pilipili usiyoila yakuwashiani?” Maana yake pilipili inayomwasha mtu ni ile aliyoila; asiyoila haiwezi kumwasha. Methali hii hutumiwa kumnasihi mtu asiyaingilie mambo yasiyomhusu. Natamani kama wahusika wangesoma makala haya kwa tafakuri (mawazo mazito; taamuli, mazingatio.)

Wahenga walisema “Siri ya mtungi iulize kata” wakiwa na maana mtungi na kata huhusiana sana. Kwa hiyo siri ya mmoja anaifahamu mwenzake.

Methali hii hutumiwa kutukumbusha kuwa tuzitakapo habari zinazomhusu mtu fulani tunapaswa kumuuliza rafiki yake wa karibu sana.

Wakati wa usajili wa wachezaji wa kandanda nchini, kila klabu huwa na wachezaji waliokusudiwa kusajiliwa na timu mbalimbali. Simba na Yanga ndizo hushindana katika usajili, na timu yenye uwezo mkubwa wa hela ndio huwavutia wachezaji.

Ili kufanikisha usajili, viongozi wa vilabu hujadiliana kuhusu wachezaji wanaofaa kusajiliwa. Jambo hili hufanyika kwa siri na baada ya kukamilishwa ndipo hutangazwa rasmi kuwa mchezaji au wachezaji fulani wamesajiliwa na Simba au Yanga.

Sivyo ilivyo kwa Simba na Yanga. Kila moja huweka hadharani majina ya wachezaji wanaokusudiwa kusajiliwa na timu hizo na magazeti huweka hadharani. Siri huwa si siri tena!

Hali kama hii huwapa nafasi wachezaji wanaotakiwa na vilabu hivyo kuchagua penye hela nyingi ingawa wengine hujiunga na klabu wanayoipenda kwa moyo wote. Tumeona na twaendelea kuona jinsi Simba na Yanga zinavyozidiana maarifa na uwezo katika usajili.

Kwa nini? Kwa sababu siri za usajili hutoka nnje mapema na kuunufaisha upande mwingine unaochukua hatua za haraka kuhitimisha usajili wa mchezaji anayetakiwa na upande mwingine.

Ukiangalia idadi ya wachezaji mahiri waliotakiwa na Yanga, sasa wametwaliwa na Simba na ndiwo wanaozitetemesha timu zingine uwanjani ikiwamo Yanga.

Yalisemwa na wahenga kuwa “Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako.” Methali hii yatufunza umuhimu wa kutochelewa tuamuapo kufanya jambo fulani.

Mvutano wa usajili kati ya Simba na Yanga husababishwa na viongozi wasiokuwa na ‘vifua’ vya kuficha siri zao. Hudhani kufanya hivyo ni ‘sifa’ kumbe wanajikaanga kwa mafuta yao wenyewe!

Huwa najiuliza: mtu anapotarajia kumposa msichana fulani hutangaza hadharani kabla ya kukubaliana naye? Unapotangaza kabla ya kukubaliana hujui kuwa unawazindua wenzako waliokuwa na lengo hilo hilo?

Kwa sababu hiyo wenzako watachukua hatua mujarabu (yenye kufaa kutengenezea jambo au kutatulia tatizo) kumpata msichana huyo na kukuwacha kwenye mzubao (hali ya kuemewa inayopelekea mtu kushindwa kufanya jambo upesi; bumbuazi.)

Kwa upande mwingine wachezaji wanapaswa kuwa makini sana wanaposajiliwa. Wanapaswa kuwa na wanasheria wao watakaowaongoza kabla ya kukubaliana na kusaini mikataba na vilabu vinavyowataka.

Mkataba ni makubaliano rasmi ya maandishi baina ya pande mbili. Kwa muktadha huu ni kati ya wachezaji wanaosajiliwa na vilabu vinavyowasajili.

Wanaosajiliwa wahakikishe wanalipwa fedha taslimu za usajili na kutokubali kulipwa kwa mafungu. Aidha vilabu lazima vifanye usajili makini na kufuata mkataba ili kuepuka malalamiko na kushitakiwa na wachezaji kwa kutolipwa mishahara kila mwezi.

Wachezaji ni waajiriwa yaani wafanyakazi kama wengine.

Vilabu vinaposhindwa kulipa mishahara ya wachezaji wao kila mwezi wataendeshaje maisha yao ya kila siku? Matokeo yake ni wachezaji kucheza wakiwa na dukuduku (joto la moyo linalosababishwa na kuudhika) kwa kutolipwa mishahara yao ya kila mwezi.

Habari Kubwa