Tukijiandaa mapema, uhaba wa vyumba vya madarasa kwa heri

31Dec 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Tukijiandaa mapema, uhaba wa vyumba vya madarasa kwa heri

KILA mwaka idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kwa ajili ya kujiunga na kidato cha kwanza inafahamika, lakini kila Desemba na Januari huwa kuna changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya maeneo wanafunzi wanaanza kidato cha kwanza bila majengo na wengine kukosa madawati kutokana na uhaba.

Nakumbuka changamoto kama hii ilijitokeza Januari mwaka huu, kwa baadhi ya shule za msingi kusoma hadi saa sita na baadaye wanafunzi wa sekondari, huku shule nyingine kama Kibasila jijini Dar es Salaam zikigawanywa na kubakiwa na vyumba vya madarasa machache.

Kila kona ya nchi ilielezwa kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kukosa shule za kusoma licha ya kupangwa kwenye shule husika, huku wengine wakikosa vyumba vya madarasa.

Mwaka huu tena hali imekuwa ile ile na sasa halmashauri mbalimbali zinakimbizana kujenga vyumba vya madarasa, kutengeneza madawati na mahitaji mengine na kuifanya shule ikamilike kwa kiwango cha chini.

Hivi karibuni Tamisemi walitangaza idadi ya wanafunzi waliokosa nafasi kidato cha kwanza kuwa ni 58,699 kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa.

Kwa sasa kuna kampeni na kauli mbalimbali ikiwamo amri kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu anapata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza.

Muungwana najiuliza kwanini suala hili linakuwa zimamoto kila mwaka, wakati wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza au wanaofika darasa la saba wanajulikana idadi yao kwa maana ya walioko shule binafsi na za umma?

Kwanini kila mwaka iwe ni kukimbizana dakika za mwisho na kuchukua hatua dakika za mwisho?

Kwa mfano, uamuzi wa kubadili muundo wa elimu kutolewa kutwa nzima na badala yake nusu siku ili kuwezesha wanafunzi kupishana kwenye majengo machache yaliyopo!

Licha ya halmashauri kuwa na majukumu mengi ya kusimamia shughuli za umma, lakini inapaswa kuwa na mpango endelevu kulingana na wanafunzi wanaomaliza kidato husika, vinginevyo kila mwanzo wa mwaka itakuwa zimamoto.

Ni vyema halmaushari zikatenga fungu au mfuko wa ujenzi wa shule za sekondari kwa makadirio ya idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuhakikisha kama inatakiwa kuongeza darasa moja kila kata inafanyika hivyo kwa ujenzi nafuu wenye kubana matumizi.

Zipo halmashauri zimefanikiwa kujenga nyumba vya madarasa kwa gharama nafuu na kwa kutumia mafundi wa jamii, kiasi cha kuwawezesha kuondokana na changamoto ya uhaba wa nyumba vya madarasa.

Zimamoto inayoonekana sasa inawapa cha kusema wanasiasa kwenye majukwaa badala ya kwenda kwenye hoja za msingi ambazo hawajatekeleza katika majimbo yao wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Takwimu za wanafunzi wanaoandikishwa na wanaofanya mtihani wa darasa la saba zipo, maana yake toka wakati huo ni kiasi cha wahusika kujipanga vyema kuhakikisha hakuna mwanafunzi anakosa darasa.

Lakini kwa kukimbizana huku ndiyo maamuzi ya kugawa shule za msingi huku matundu ya vyoo yakiwa ni yale yale, na shule kupoteza ubora wa elimu inayotolewa.

Shule nyingi za ‘zimamoto’ huwa elimu yake haina ubora unaotakiwa, zaidi ya kuhakikisha kila mtoto amekwenda shule ili ionekane hakuna aliyebaki nyumbani.

Watoto wengi wa kike wamekuwa waathirika wa ugonjwa wa UTI unaosababishwa na matumizi ya vyoo visivyofaa, na kwamba mazingira ya kuchanganya matumizi ya choo kwa wanafunzi wadogo na wakubwa maana yake ni kuwaumiza wote na sana sana wadogo.

Akili ya mwanafunzi wa darasa la awali au la kwanza haiwezi kuwa sawa na ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza na ndiyo maana lazima wawe na vyoo vyao.

Lazima Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu wawe na utaratibu maalum wa kuhakikisha majengo yanakuwapo kusubiri wanafunzi na si kusubiri wanafunzi wafaulu na ndiyo wasubiri majengo yajengwe.

Habari Kubwa