Kijana matatani kwa tuhuma za kukutwa na sare za jeshi

31Dec 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Kijana matatani kwa tuhuma za kukutwa na sare za jeshi

KIJANA aliyetajwa kwa jina la Isaka Jakobo (20) mkazi wa Kijiji cha Shigamba, katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ulrich Matei, alisema mtuhumiwa alikamatwa Disemba 27, mwaka huu, saa 9:00 alasiri.

Alizitaja sare alizokamatwa nazo kijana huyo kuwa ni nishani mbili, mkanda mmoja wa mkuu wa utii na nidhamu (RSM), mkanda mmoja wa kawaida na kofia mbili ambazo mbili zina krauni zenye rangi ya kijani na moja yenye rangi nyekundu, na begi moja la mgongoni.

Matei alisema kijana huyo alikutwa na sare hizo akiwa amezipakia kwenye pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC852 BLE na kwamba bado uchunguzi unaendelea ili kujua alikozichukua na alikokuwa anazipeleka.

Alisema baada ya uchunguzi wa awali, jeshi hilo lilibaini kuwa pikipiki aliyokuwa anaitumia kijana huyo nayo ni ya wizi.

"Kijana huyo alikamatwa na askari waliokuwa kwenye doria katika eneo hilo baada ya kuwa na wasiwasi naye na walipochunguza walibaini kuwa alikuwa amebeba sare za jeshi. Sasa hatujui alikozitoa na alikuwa anakwenda kufanyia nini lakini tunaendelea kumhoji," alisema Matei.

Pia alisema jeshi hilo linaendelea na misako katika maeneo mbalimbali ya Mbeya kwa ajili ya kukamata bidhaa zinazoingizwa nchini kinyume cha sheria zikiwamo pombe kali kutoka Zambia na Malawi.

Habari Kubwa