Lipumba adai uchumi ulikuwa mgumu 2019

31Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Lipumba adai uchumi ulikuwa mgumu 2019

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amedai mwaka 2019 ulikuwa mgumu kiuchumi na kisiasa nchini.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuwatakia kheri ya mwaka mpya Watanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho, Zainabu Mndolwa na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Jafar Mneke. PICHA: JUMANNE JUMA

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari, ujumbe mkuu ukiwa salamu za chama kwake kwa wananchi kufunga mwaka.

Alidai mwaka unaoisha leo ulikuwa na kile alichokiita shida kiuchumi kutokana na biashara kupungua na ajira kuwa duni, akitoa rai kwa wahusika kuweka ngumu katika kuhakikisha yanafanyika mapinduzi kwenye sekta ya kilimo ili kukuza uchumi.

Prof. Lipumba ambaye ni mbobezi katika masuala ya kiuchumi, alieleza kuwa takwimu za serikali zinaonyesha idadi ya watu maskini imeongezeka kutoka watu milioni 13 mwaka 2007 hadi kufikia milioni 14 mwaka  2018.

"Nusu ya Watanzania wamo katika dimbwi la umaskini, Tanzania inahitaji kutokomeza umaskini kwa kuleta mapinduzi kwenye kilimo. Kilimo cha korosho wameathirika na sera za serikali zilivyotekelezwa katika ununuzi wa korosho na baadhi yao hawajalipwa msimu wa mwaka 2017 na 2018.

"Wakulima wa tumbaku wamekosa soko baada ya mnunuzi mkubwa kuacha kushiriki kwa madai ya tozo na kodi kubwa," alidai.

Aliendelea kueleza kuwa mwaka 2019 ulikuwa mgumu wa kimaisha kwa Watanzania kwa kuwa kauli za 'vyuma kukaza' zilitawala zaidi, na kwamba taarifa za furaha duniani kwa mwaka 2019 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya nne kati ya 156 kwa kukosa furaha.

"Ugumu wa biashara umepunguza kampuni mpya za biashara zinazosajiliwa nchini kutoka 8,890 mwaka 2015 hadi kufikia 5,276 mwaka 2018. Rwanda, kampuni mpya zilizosajiliwa ni 10,635 mwaka 2018 na mwaka 2015 walisajili kampuni 9,775," alidai.

DEMOKRASIA

Prof. Lipumba pia alidai Tanzania imerudi nyuma katika ujenzi wa demokrasia, akitolea mfano matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa aliyodai zaidi ya asilimia 90 ya wagombea wa chama chake waliojitokeza katika vitongoji, vijiji na mitaa walinyimwa nafasi ya kugombea.

“Tulilazimika kutoshiriki uchaguzi baada ya wagombea wetu kuondolewa pia vyama vingine vya upinzani havikushiriki baada ya kunyimwa fursa.

“Ushiriki wa wananchi katika kuamua mambo yanayogusa maisha yao ni suala muhimu la maendeleo endelevu. Ni muhimu serikali ikatambua ujenzi wa demokrasia ni sehemu muhimu ya maendeleo," alishauri.

Prof.Lipumba pia aliitaka serikali kufanyia kazi kile alichokiita tatizo la watu kupotea katika mazingira yenye utata, akitolea mfano watu mbalimbali waliopotea katika mazingira hayo.

Prof. Lipumba pia alizungumzia uchaguzi mkuu ujao, akieleza kuwa CUF inajipanga kuweka wagombea nchi nzima katika ngazi zote, huku akisisitiza umuhimu wa nchi kuwa na tume huru ya uchaguzi.

“Hii ni nchi yetu, ni wajibu wetu kushiri katika uchaguzi mkuu 2020 na tuchague viongozi watakaojenga amani, kujenga haki na uchumi utakaoongeza ajira na kuwapa furaha wananchi wote, sote tuwe ngaringari katika kudai uchaguzi huru na haki mwaka 2020,” alisema.

Habari Kubwa