Waziri ataka matamasha msimu wa utalii

31Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waziri ataka matamasha msimu wa utalii

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amewataka wadau wa utalii kuhakikisha  wanafanya matamasha ya kukuza na kuendeleza sekta hiyo wakati wa msimu wa utalii.

Kwa kufanya hivyo watawafanya watalii kushiriki katika matamasha hayo licha ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Akizungumza juzi wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Utalii la Lamadi litakalomalizika kesho katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Kanyasu alitaka tamasha hilo lifanyike katika kipindi kijacho wakati wa mfumuko wa watalii ili watalii wote  wanaotoka katika  Hifadhi ya Taifa ya  Serengeti washiriki.

Alisema lengo la tamasha hilo ni  kuwafanya watalii kushiriki moja kwa moja kupitia ngoma za asili, mavazi ya kitamaduni na vyakula vya kiasili hali inayowafanya watalii  kukaa kwa muda mrefu nchini.

Kanyasu alisema tamasha hilo lina umuhimu kwa vile linatoa fursa kwa watalii baada ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyo karibu na wilaya hiyo  kupata fursa ya  kujumuika na jamii kupitia utamaduni wa makabila mbalimbali nchini.

Kanyasu aliwataka waandaaji hao kuliandaa tamasha hilo  kwa kuvialika vikundi  vya ngoma kutoka pande mbalimbali za nchi badala ya kuwa na vikundi vichache vya kutoka sehemu moja.

Katika hatua nyingine, Kanyasu amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, kwa kuwa na  mawazo ya kuanzisha tamasha hilo ambalo litachagiza utalii kwa wananchi wa kawaida baada ya watalii kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Aliwataka wakuu wa wilaya zingine kuandaa matamasha ya utalii kwa ajili ya kukuza utalii katika wilaya zao, hali  itakayosababisha watalii kukaa muda mrefu, hivyo kusababisha jamii kunufaika.

Kwa upande wake, Mwera ambaye ni mwenyekiti wa tamasha hilo, alisema tamasha hilo litachagiza utalii wa ndani  na kuwafanya wananchi kuwa mabalozi wa vivutio vya utalii.

Pia alisema tamasha hilo litasaidia kuamsha ari ya wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushiriki kwenye shughuli za utalii hali itayowasaidia kujiongezea kipato.

Habari Kubwa