Walimu 16,000 kuajiriwa mwakani

31Dec 2019
Renatha Msungu
DODOMA 
Nipashe
Walimu 16,000 kuajiriwa mwakani

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatarajia kuajiri walimu 16,000 katika mwaka ujao wa kalenda ili kukidhi tatizo la uhaba wa walimu hususan wa Sayansi katika shule mbalimbali nchini. 

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, William Ole Nasha, wakati akijibu swali kuhusiana na upungufu wa walimu wa Sayansi katika Shule ya Viba iliyopo Igunga mkoani Tabora. 

Nasha alisema mpango huo wa kuajiri utatekelezwa ndani ya miaka mitatu, lengo ikiwa ni kutatua changamoto ya ukosefu wa walimu hususan wa Sayansi. 

Alisema mikakati walioiweka ni kuhakikisha wanaajiri  ambao wanahitimu kutoka vyuoni ili kwenda kuziba mapengo yanayohitajika.

"Kuna vyuo maalum ambavyo tumevitenga kwa ajili ya kutoa walimu wa Sayansi hii itatusaidia sana," alisema Ole Nasha. 

"Lakini ukumbuke wanaoajiri ni Tamisemi, Wizara ya Elimu tunasema uhaba tulionao Tamisemi kazi yao kuajiri," alieleza.

Alisema wao wanapeleka walimu katika shule kulingana na uhitaji wa sehemu husika. 

Alisema moja ya changamoto iliyochangia upungufu wa walimu ni walimu waliokutwa na vyeti feki na kuondolewa. 

Alisema kulikabili suala hili itachukua muda, lakini litatatulika ndani ya miaka mitatu hadi minne ambayo wanaendelea kuajiri. 

"Tutaendelea kuajiri, kufundisha na kuboresha miundombinu kwa walimu ambao wanaajiriwa," alisema Ole Nasha. 

Habari Kubwa