Yanga yapangua gia msimamo Ligi Kuu

31Dec 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yapangua gia msimamo Ligi Kuu
  • ***Tariq aanza kwa bao, nafasi tatu moja atupia, waishusha Kagera Sugar na kukaa nyuma ya Simba huku...

STRAIKA mpya, Tariq Seif, aliyesajiliwa kipindi hiki cha dirisha dogo akitokea nchini Misri alikokwenda kucheza soka la kulipwa, amepeleka furaha Yanga baada ya kufunga bao pekee dakika ya 84 lililoiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa 1-0-

-dhidi ya Biashara United kutoka mkoani Mara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Hata hivyo, mchezaji huyo ambaye ni mechi yake ya kwanza kucheza, akifanikiwa kufunga bao lake la kwanza, hakushangilia bao hilo, badala yake aliweka mikono juu kuomba radhi, kutokana na kuifunga timu yake ya zamani aliyoichezea kabla ya kutimkia Uarabuni.

Ushindi huo, unaifanya Yanga kuanza kupangua gia za msimamo wa Ligi Kuu Bara, ambapo sasa imefikisha pointi 24 baada ya mechi 11, hivyo kuishusha Kagera Sugar hadi nafasi ya tatu licha ya kucheza mechi 14, lakini timu hizo zikiwa na pointi sawa ila Wanajangwani hao wakinufaika na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Lilikuwa ni bao lililowapa faraja mashabiki wa Yanga ambao tayari walishaanza kukata tamaa na kuona kuwa huenda wangelazimishwa sare ya bila kufungana.

Tariq, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya David Molinga, kabla ya bao hilo alipata nafasi mbili, moja akishindwa kulenga lango na nyingine ikipanguliwa na kipa wa Biashara United, Daniel Mgore kabla ya baadaye kupokea krosi safi kutoka kwa mchezaji ambaye pia aliingia kipindi cha pili, Papy Tshishimbi na kuandika bao hilo pekee.

Awali ilikuwa ni kichwa chake kilishindwa kulenga lango, lakini katika dakika ya 60 alipiga kichwa cha kudundisha, na kipa wa Biashara, Mgore aliruka juu na kuupangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mbali na Tariq, Yanga ilimchezesha mchezaji mwingine aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo akitokea JKT Tanzania, Adeiyum Saleh.

Kipindi cha kwanza kilikuwa ni cha kupooza kwa timu zote mbili, huku Yanga ikipata nafasi mbili tu za wazi ambazo ilishindwa kuzitumia.

Lakini kipindi cha pili Biashara ilitumia muda mwingi kucheza nyuma ya mpira, huku ilikionekana kuzuia zaidi kuliko kushambulia na hilo ndilo lililowaponza.

Biashara ilifanya shambulio kali moja tu, dakika ya 48 wakati Bright Obina alipopiga shuti lililotoka pembeni kidogo ya lango.

Kwa matokeo hayo, Yanga sasa inakaa nafasi ya pili nyuma ya Simba, wakati huu timu hizo zikijiandaa kukutana Jumamosi katika uwanja huo, hata hivyo Kagera Sugar yenye pointi 24, ingeweza kuendelea kung'ang'ania kukaa nafasi pili, lakini jana ilishindwa na kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Lipuli ikiwa nyumbani, Uwanja wa Samora mjini Iringa imeiangamiza Mbao FC mabao 3-0, Coastal Union ikiendeleza wimbi la ushindi Uwanja wa Mkwakwani kwa kuichapa Mbeya City mabao 2-0, Mtibwa Sugar ikiduwazwa bao 1-0 nyumbani Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya Alliance FC.

Habari Kubwa