Simba: Ndanda daraja la Yanga

31Dec 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba: Ndanda daraja la Yanga

MECHI muhimu! Hayo ni maneno ya Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC kutoka mkoani Mtwara inayotarajiwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Baada ya mechi ya leo, Simba ambao watakuwa wenyeji, itaingia kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya watani zao, Yanga utakaochezwa Jumamosi kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Matola, alisema wamejiandaa kupata ushindi katika mechi ya leo ambayo itakuwa ni sehemu pia ya maandalizi kuelekea mchezo wao dhidi ya Yanga.

Matola alisema kiufundi, mechi hizo ni tofauti, lakini wamejipanga kuingia uwanjani kwa tahadhari kwa sababu wanahitaji kuondoka na pointi tatu muhimu.

Alisema kila mchezaji yuko tayari na wanajua Ndanda wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili waondoke kwenye janga la kushuka daraja.

"Ni mechi muhimu sana kwetu, tunahitaji kushinda ili kuendelea kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi, tunaiangalia Ndanda kwanza, halafu itafuata Yanga, ingawa tukipata matokeo ya ushindi, yataimarisha nguvu ya timu," alisema Matola.

Nahodha huyo wa zamani Simba aliongeza kuwa kila mechi kwao ni sawa na fainali, hivyo wamewaandaa wachezaji kupambana katika dakika zote.

Abdul Mingange, Kocha Mkuu wa Ndanda FC, alisema anaifahamu vema Simba na amewaandaa nyota wake 'kubana njia' ambazo wanazitumia katika kutengeneza mabao.

"Nimewaangalia Simba mechi zao zote, ninajua mahali ambapo wana upungufu, kama tutafanikiwa kuwabana kama tulivyowasoma, naamini tutapata matokeo mazuri, tunahitaji ushindi, ligi haina mwenyewe, hata nyumbani kwao tunaweza kuwasumbua," alisema Mingange.

Aliongeza kuwa amewataka wachezaji wake kutofikiria matokeo ya mechi zilizopita, kwa sababu kikosi cha msimu huu, si walichocheza nacho msimu uliopita.

Simba ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 12, wakati Ndanda FC yenye pointi nane imeshacheza michezo 13, iko katika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.

Habari Kubwa