Likizo yakwamisha kesi ya Zitto

04Jan 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Likizo yakwamisha kesi ya Zitto

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, baada ya hakimu anayeisikiliza kwenda likizo.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa hoja za pande zote mbili za kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Hata hivyo, kwa kuwa Hakimu Huruma Shaidi, anayesikiliza kesi hiyo yuko likizo, Hakimu Chaungu alisema itaendelea kusikilizwa Januari 10, mwaka huu.

Awali mahakamani hapo, Upande wa Jamhuri uliita mashahidi 14 kuthibitisha makosa ya uchochezi dhidi ya Zitto.

Katika kesi hiyo, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, akidaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya ACT-Wazalendo.

Habari Kubwa