Lori lingine la mafuta lalipuka

04Jan 2020
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Lori lingine la mafuta lalipuka

LORI la mafuta, mali ya Kampuni ya World Oil ya jijini Dar es Salaam, lililokuwa linasafirisha mafuta ya petroli kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia, limeteketea kwa moto na kujeruhi watu wawili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alidai jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 10:30 jioni katika eneo la Meta-Igurusi wilayani Mbarali katika Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam).

Alilitaja gari lililoteketea kuwa ni aina ya Scania Tanker lenye namba za usajili T 956 DRT na tela namba T 886 DRV ambalo lilikuwa linaendeshwa na Issa Yusuph (35), mkazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Kamanda Matei aliwataja waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Julius Daud (30) na Stanford Mwakyusa (45), wote wakazi wa Kata ya Igurusi wilayani Mbarali ambao walienda kwa ajili ya kusaidia kuhamisha mafuta kutoka kwenye gari hilo baada ya kuharibika.

Alidai kuwa awali gari hilo liliharibika katika eneo hilo Januari Mosi, mwaka huu na baada ya matengenezo kushindikana, waliamua kuhamishia mafuta kwenye gari lingine lenye namba za usajili T 844 AWJ.

“Waliojeruhiwa ndiyo waliokuwa wanafanya kazi ya kuhamisha mafuta kwenye gari hiyo kwa kutumia mashine ya kusukuma maji (water pump). Sasa, wakati wanaendelea na kazi ulitokea mlipuko kwenye hiyo mashine na kusababisha moto mkubwa ambao uliteketeza gari hilo na kuwajeruhi,” alidai.

Kamanda Matei alidai kuwa mbali na gari hiyo kuteketea, pia kulitokea uharibifu kwenye magari mawili ambayo mafuta yalikuwa yanahamishiwa pamoja na gari la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya lenye namba za usajiri SM 4633 ambalo lilikuwa linatumika kuzima moto huo.

Kamanda Matei alisema majeruhi wa ajali hiyo waliwahishwa katika Kituo cha Afya cha Kata ya Igurusi kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha waliyoyapata kwenye ajali hiyo.

Aliwataka wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuepuka kusogea kwenye maeneo ambayo wanaona kuna hatari ya mafuta kulipuka kwa maelezo kuwa ajali za aina hiyo zinakuwa na madhara makubwa.

Mwaka jana, ajali ya moto ilitokea katika eneo la Msamvu Itigi mkoani Morogoro wakati wananchi walipokuwa wanachota mafuta yaliyokuwa yanamwagika baada ya lori la mafuta kuanguka. Zaidi ya watu 100 walifariki dunia katika ajali hiyo na kuwa miongoni mwa matukio ya hatari zaidi kuwahi kutokea mwaka 2019.

Habari Kubwa