Ama zao, ama zetu

04Jan 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Ama zao, ama zetu
  • ***Sven, Mkwasa kila mmoja atamba kikosi chake kimejipanga kuondoka na ushindi katika mtanange huo...

TAMBO na majigambo yaliyokuwa yanatawala kutoka kila kona ya mashabiki na wanachama wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga yanatarajiwa kumalizika baada ya vigogo hao kukutana katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ambayo itachezeshwa na "mwanadada", Jonesia Rukyaa, kutoka Bukoba mkoani Kagera, ni ya kwanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/20, na pia ni ya kwanza kwa mwaka huu mpya wa 2020.

Simba ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Bara watashuka uwanjani leo wakiwa na rekodi ya ushindi wa mechi tatau mfululizo za ligi hiyo dhidi ya Lipuli FC, KMC FC na Ndanda FC, wakati Yanga ilitoka sare ya bila kufungana ugenini dhidi ya Mbeya City na imeshinda michezo miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Biashara United.

Wekundu wa Msimbazi ambao wamecheza mechi 13, wana pointi 34 wakati Yanga ambayo imecheza mechi mbili pungufu iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye kushirikisha timu 20 ikiwa imejikusanyia pointi 24.

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara watashuka uwanjani pia wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0, walilopata katika mchezo wa marudiano walioupata msimu uliopita.

Akizungumza jijini jana, kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, Sven Vandenbroeck, alisema kuwa kikosi chake kiko tayari na imara kwa ajili ya mchezo huo na anaamini watapata matokeo mazuri.

Sven alisema kuwa anajua mechi ya watani wa jadi huwa na matarajio makubwa kwa kila upande, lakini kwake amekiweka vema kikosi chake ili kutimiza malengo waliyonayo ya kuwania ubingwa.

"Ni mechi ambayo pia inatoa taswira ya mbio za kuwania ubingwa, kikosi changu kiko imara, wachezaji wote wamefanya mazoezi vizuri isipokuwa Miraji (Athumani) na Rashid Juma, waliobaki wote wako tayari kwa mchezo wa kesho (leo)," alisema kocha huyo ambaye ataiongoza kwa mara ya kwanza Simba dhidi ya Yanga.

Naye nahodha wa Simba, John Bocco, alisema kuwa wanatarajia kupata ushindi katika mchezo huo kwa sababu kikosi cha timu yao kinaundwa na wachezaji wenye uzoefu na mechi 'kubwa' na zenye ushindani.

"Tuna muunganiko mzuri ndani ya uwanja na nje ya uwanja, sina mashaka kabisa na mchezo wa kesho, tunawaomba mashabiki wetu waendelee kuwa na imani na sisi, kikubwa tutaenda kupambana kwa ajili ya timu yetu ili tuweze kupata pointi tatu muhimu," alisema nahodha huyo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Azam FC, alisema kuwa watashuka uwanjani kupambana kwa ajili kuweka heshima ya timu na wao wachezaji.

Kocha Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema mechi ya leo ni ya kawaida kama ilivyo michezo mingine ya kawaida, lakini inatofautishwa na klabu zake kuwa na mashabiki wake.

Mkwasa alisema kuwa malengo yao ni kupata ushindi katika mchezo huo na kikosi chake kina rekodi nzuri katika mechi zake mbili zilizopita.

Alisema kuwa kikosi chake kimejiandaa kupambana kupata ushindi na ameweka wazi kwamba mechi ya leo haitakuwa nyepesi kama wapinzani wanavyofikiria.

"Mechi mbili za mwisho, tumecheza na timu ambayo haijafungwa, sisi ndio tumefungua 'duka', wasifikirie Yanga ni timu nyepesi, na timu rahisi, mechi za Simba na Yanga, sio ngeni kwangu mimi, nimeweza kuwafunga nikiwa mchezaji, wamenifunga nikiwa mchezaji na kocha," alisema Mkwasa.

Aliwataja wachezaji ambao watakosa mechi ya leo ni beki, Lamine Moro, mwenye kadi tatu za njano, pamoja na mshambuliaji Tariq Seif, ambaye ni majeruhi.

"Tumetoka kwenye ratiba ngumu, tumesafiri umbali mrefu, tunaiheshimu mechi hiyo, tumepata matokeo mazuri katika mechi mbili ngumu zilizopita, tunataka kuendeleza ushindi kwa kuwafunga Simba na kusitiza rekodi yao ya kucheza michezo mingi bila ya kufungwa," Mkwasa alisema.

Baada ya mechi ya leo, vigogo hao watasafiri kuelekea Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia keshokutwa visiwani humo kwa kushirikisha timu za hapa nchini.

Habari Kubwa