Riba kubwa mikopo zamkwaza Mpango

08Jan 2020
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Riba kubwa mikopo zamkwaza Mpango

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameshtukia riba kubwa inayotozwa na taasisi za fedha ambazo amesema zinawaumiza wananchi.

Sambamba na hilo, awewataka watumishi wa umma ambao wanaendesha maeneo ya huduma ndogo za fedha kuacha mara moja kabla serikali haijawabaini na kuwachukulia hatua kali.

Dk. Mpango aliyasema hayo jijini hapa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uendeshaji wa huduma ndogo za fedha nchini ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa utozaji wa riba kubwa kwa wananchi.

Alisema kuwa moja ya changamoto nchini katika uendeshaji wa huduma ndogo za fedha ni riba kubwa za mikopo ambazo zimekuwa zikitolewa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Alisema hivi sasa watoa huduma ndogo za fedha, wamekuwa na tabia ya kujipangia riba vile wanavyotaka ili kujipatia faida kwa haraka bila kujali wananchi wanaowakopesha.

"Huduma ndogo ya fedha nchini imekuwa kikwazo kwa wananchi wengi. Unakuta leo watu wanamkata mtu riba karibia hata mshahara wake mzima, hivyo lazima ufanyike utaratibu ambao utasaidia kuondoa suala hili. Lakini watumishi wa umma ambao wanaendesha huduma hizi wajitoe mara moja kwani haiwezekani wao ndiyo wawe wanawaumiza wenzao," alisema Dk. Mpango.

Dk. Mpango alimwagiza Gavana wa Benki Kuu (BOT) kuhakikisha kuwa anaitisha mkutano wa nchi nzima utakaowajumuisha watoa huduma wote wa huduma ndogo za fedha.

"Lazima Gavana, uwaite watu wote wanaotoa huduma ndogo ya fedha ili mjadiliane nao namna ya uendeshaji wa huduma hizi. Si watu kutaka kutajirika kupitia migongo ya Watanzania maskini, lazima riba iwe nafuu kwa mkopaji ili ajikwamua kiuchumi na sio kunyonywa kama ilivyo sasa," alisema Dk. Mpango.

Kuhusu changamoto ya utengenezaji na usambazaji wa fedha bandia, Dk. Mpango alisema hilo ni jambao ambalo linamuumiza sana kwa kuwa linaathiri uchumi wa nchi.

"Mimi hawa watu ingekuwa maamuzi (uamuzi) yangu (wangu) ningekata mikono yao… wakati sisi tunapambana kupandisha uchumi wa nchi mtu mwingine anaingiza fedha bandia katika mzunguko. Huyo hana tofauti na yule ambaye mpo naye kwenye mtumbwi halafu anautoboa," alisema.

Habari Kubwa